Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara
Vikundi
vya Huduma ndogo za fedha pamoja na Wafanyabiashara mbalimbali kutoka
Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wameshiriki katika mafunzo ya utunzaji
fedha yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi za
Fedha pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mafunzo
hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara, na
kushirikisha wafanyabiashara na wananchi zaidi ya 500 kutoka maeneo
mbalimbali.
Akizungunza
kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara
Wanawake Tanzania -TWCC Mkoa wa Mtwara, Bi.Mwajuma Oankoni, alisema
kuwa elimu hiyo imekuja wakati muafaka na italeta manufaa kwa wananchi.
"Mimi
kama mfanyabishana na kiongozi wa wafanyabiashara wanawake katika mkoa
wa Mtwara, napongeza sana juhudi hizi za serikali, elimu ya fedha
inahitajika sana katika mkoa wetu kutokana na wengi wetu kufanya mambo
kwa mazoea " alisema Bi. Mwajuma
Kwa
upande wake mfanyabiashara Bi. Mwajuma Issa, alisema kuwa elimu
iliyotolewa itawasaidia kutunza fedha katika taasisi rasmi, ili ziweze
kuwasaidia kwa matumizi ya muda mrefu.
"Sisi
tumezoea mtu ukipata hela unaziingiza kwenye matumizi zote, tena
matumizi yenyewe ni ya shughuli za unyago na sherehe zingine, hali
ambayo imekuwa ikizidisha umasikini kwa wananchi wengi hivyo elimu hii
itatusaidia kuepukana na hilo" alieleza Bi. Mwajuma
Awali
akizungumzia mafunzo hayo, Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya
Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro
alieleza kuwa lengo ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya
fedha kwa ujumla.
"Programu
hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali
ya mkoa wa Mtwara, ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya
kupata huduma za kifedha na namna ya kuzisimamia fedha zao kwa ajili ya
kuwaletea maendeleo. alisema Kimaro.
0 comments:
Post a Comment