Home » » HALMASHAURI YA MJI NANYAMBA KUJENGA SHULE KUBWA YA UFUNDI.

HALMASHAURI YA MJI NANYAMBA KUJENGA SHULE KUBWA YA UFUNDI.

Halmashauri ya Mji Nanyamba inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule ya ufundi stadi itakayojengwa katika mtaa wa Nanyamba B Kata ya Nanyamba kwa ufadhili wa SEQUIP.

Taarifa kamati ya Fedha, Utawala na Mipango iliyowasilishwa Leo tarehe 31/07/2024 katika Baraza la Madiwani ilieleza kuwa tayari Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nanyamba (WDC) imefanikiwa kulipa fidia na kutwaa eneo lenye ukubwa ekari 10 kwa gharama ya shilingi 20,000,000 (Milioni ishirini) inayotokana na michango ya shilingi ishirini iliyokatwa kwa wakulima wa korosho.

“Itakuwa ni shule kubwa ambayo itakuwa na mabweni, karakana, maabara na itakusanya wanafunzi wa Halmashauri yote. Mwanafunzi akihitimu pale kutakuwa na cheti cha taaluma pamoja na cheti cha ufundi.” Alieleza Mhe. Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba.

Katika hatua nyingine madiwani wamepiga kura za kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ambapo Mhe. Maliki Hamis Majali, Diwani wa kata ya Kiromba amepigiwa kura za Ndio kuendelea na nafasi yake hiyo.

Aidha, Mhe. Jamal Abdallah Kapende, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba ametangaza kamati mpya za kudumu zitakazoanza kazi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa