Home » » WANANCHI TANDAHIMBA WAFIKIWA NA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA

WANANCHI TANDAHIMBA WAFIKIWA NA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA

Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara

Wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Halamshauri ya Wilaya ya Mtwara, wameendelea kupata elimu ya matumizi sahihi ya fedha ambayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha, yakihusisha Wilaya zote za mkoa wa Mtwara

Katika mafunzo yaliyofanyika katika Kijiji Cha nanhyanga, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, wajasiriamali na wafanyabishara  walijitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo huku wengi wao wakikiri kuwa wamejifunza mambo mengi ambayo walikuwa hawayajui kabla.

Akizungumzia programu hiyo, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha - Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, ameeleza kuwa Wizara ya Fedha inafanya jambo ambalo lilihitajika kwa wananchi kwa muda mrefu akisisitiza kuwa sasa kutakuwa na mwamko mpya.

“Wananchi hususan wa maeneo ya vijijini wanatakiwa kuwa na uelewa wa masula muhimu ya fedha, ndio maana unaweza kukuta wana fedha nyingi kwa wakati mmoja na baada ya muda hamjui hata zilienda wapi, kupitia elimu hii itawakomboa” alisema Bi. Mnzava.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha - Wizara ya Fedha, Bw. Kelvin Kalengela, amesema Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa matumizi ya fedha kwa wananchi wake, na ndio maana wengi wao wamekuwa wakienda kukopa mikopo inayowaumiza.

“Kuna mikopo ya aina mbalimbali inatolewa kienyeji, mingi haina sifa wala vigezo lakini wananchi hawajui ndio maana tunawapa elimu ili pia wasitumie fedha zao vibaya” alieleza Bw. Kalengela.

Kwa upande wake Bi Habiba Shube Mwananchi wa Kijiji cha Tandahimba ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Taasisi zingine zinazoshiriki katika kutoa elimu hiyo akieleza kuwa itawasaidia wananchi hususan akina mama kuepuka mikopo umiza.

“Hii sisi akina mama naweza kusema inatuhusu kuliko hata wanaume, sisi ndio wahanga wakubwa maana tuna shughuli nyingi ambazo zinatumia pesa hivyo tunajikuta tunaingia kwenye mikopo isiyo na sifa tunalipa madeni, kila siku tunalipa madeni tu” Alisema mwananchi huyo.

Mafunzo haya yaliyoanza mapema wiki hii, yanaendelea katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mtwara, lengo lake likiwa  ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya fedha kwa ujumla.




0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa