KUSIMAMA KWA SHUGHULI ZA
UZALISHAJI KATIKA KIWANDA CHA DANGOTE
:
UZALISHAJI katika kiwanda cha saruji
cha Dangote kilichopo Mtwara umeathirika kwa kiasi kikubwa tokea wiki
iliyopita. Tatizo hili la muda limetokana na hitilafu za kiufundi katika
mitambo ya kiwanda. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Bwana Harpreet
Duggal amesema mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji
zitarejea katika siku chache zijazo.
Alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa
kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho jambo
lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo. Hata hivyo alizitaja
hitilafu hizo kuwa ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi
kijacho.
Alipoulizwa kuhusu gharama kubwa za
uzalishaji, Bwana Duggal alisema unapolinganisha na gharama nyingine za
uzalishaji katika Dangote, gharama za uendeshaji Tanzania ni za juu mno. Moja
ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda. Na
pia kiwanda kuwepo mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la gharama
za usafirishaji. Akasema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya
kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.
Akaongeza, “Tuna matumani makubwa
kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania na tupo makini, kwa
kushirikiana na Serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili tuweze
kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa
na bei nafuu nchini.”
Tangu kuzinduliwa kwa kiwanda cha
saruji cha Dangote, bei ya saruji nchini Tanzania imeshuka kwa zaidi ya
asilimia 30.
Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara
chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 600 kina uwekezaji mkubwa katika
saruji kuliko vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani milioni
tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1000 wa
Mtwara.
0 comments:
Post a Comment