Home » » DKT MGWATU: SIJARIDHISHWA NA UKUSANYAJI MAPATO NA MADENI.

DKT MGWATU: SIJARIDHISHWA NA UKUSANYAJI MAPATO NA MADENI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Na Theresia Mwami TEMESA Mtwara.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu amesema kuwa hajaridhishwa na ukusanyaji wa mapato na madeni katika kituo cha Mtwara katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo karakana imekusanya asilimia 20% tu ya kiasi cha pesa ilichozalisha.

Dkt Mgwatu amesema kuwa hatovumilia uzembe wowote utakaojitokeza katika suala la ukusanyaji wa mapato na madeni katika vituo vyote vya TEMESA nchini.

“Hatuwezi kuendesha vituo na karakana zetu kwa mwendo huu hivyo inatupasa kuongeza juhudi katika kufuatilia madeni” alisema Dkt. Mgwatu.

Kwa upande wake Meneja wa TEMESA Mtwara Mhandisi Said Mongomongo amesema kuwa kuna changamoto za Taasisi nyingi kutolipa kwa wakati gharama za matengenezo ya magari na mashine mbalimbali katika karakana yake.

Mhandisi Mongomongo amewataja baadhi ya wadaiwa sugu kuwa ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Ofisi ya Katibu Tawala mkoani Mtwara.

Akiwa mkoani Mtwara, Dkt Mgwatu ametembelea Kivuko cha MV. Mafanikio kinachotoa huduma ya usafiri kati ya Msangamkuu na Msemo pamoja na Kivuko cha MV. Kilambo kinachotoa huduma kati ya Kilambo (upande wa Tanzania) na Namoto (upande wa Msumbiji).

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuangalia utendaji kazi wa vituo hivyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa