Home » » JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO WAISHIO KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO WAISHIO KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

JAMII nchini imetakiwa kuona umuhimu na wajibu wa kuwalea na kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kufikia ndoto zao katika kimaisha.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Faidika Wote Pamoja (Fawopa-Tanzania), la mkoani hapa, Baltazar Komba, wakati akiwakabidhi sare za shule na viatu wanafunzi 52 wa shule za Sekondari tisa katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani, ambao wanaishi katika mazingira magumu.
“Jamii inatakiwa ione umuhimu na wajibu wa kuwalea na kuwasaidia watoto wanaishi katika mazingira magumu…Huwezi kunywa pombe za laki moja kila siku wakati nyumba ya jirani yako kuna mtoto anahitaji msaada wa kwenda shule na yuko nyumbani amekosa ada ya sh 20,000 kwa nini usimsaidie kumlipia ada?” alihoji Komba.
Komba, alisema kuwa Shirika lao lina wajibu mkubwa wa kuwasaidia watoto mahitaji ya shule, ili mwisho wa siku waweze kufikia malengo yao ya kimaisha.
Alisema kuwa msaada waliotoa, kila mtoto amepata sare za shule mbili pamoja na viatu jozi moja, lakini hapo nyuma walishawapatia msaada wa michango ya shule na madaftari.
Wanafunzi waliopatiwa msaada huo wanatoka shule za Sekondari za Shangani, Mikindani, Mitengo, Sabasaba, Bandari, Umoja, RahaLeo, Chuno na Sino.
“Msaada huu tuliotoa kwa wanafunzi 52 katika shule za sekondari tisa zilizopo katika Halmashauri yetu, tumefadhiliwa na Shirika la Social Action Fund (SATF), la jijini Dar es Salaam…Sisi kama Fawopa wajibu wetu ni kusaidia watoto waliopo katika mazingira hatarishi kwa sababu ya kuwa yatima ama mazingira magumu kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasaidia.
“Tunajua watoto waliokuwa katika mazingira hatarishi huwa wana ndoto kubwa, lakini kutokana kutokuwa na uwezo wanabaki kukata tamaa ya maisha, lakini sisi tunachokifanya ni kuwawezesha katika hilo na ndio sehemu ya kuwafanya wafikie ndoto zao,” alisema.
Kwa upande wao, Wanafunzi Hadija Ali na Dadi Namkumbe, walilishukuru shirika hilo kwa msaada huo na kuwaahidi kusoma kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa