Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Faidika Wote Pamoja
(Fawopa-Tanzania), la mkoani Mtwara, limeendesha mafunzo ya
ujasiriamali kwa wazazi na walezi wa watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi ili kuwawezesha kumudu kutunza familia zao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa
mafunzo hayo siku tatu, Katibu Mtendaji wa Fawopa-Tanzania, Baltazar
Komba, alisema lengo kubwa baada ya mafunzo hayo kumalizika ni kuunda
vikundi vya watu kumi kumi, ambao watapewa mkopo na Fawopa kwa
ufadhili wa Serikali ya Uholanzi chini ya usimamizi wa Shirika la
Maendeleo la Uholanzi la Terre Des Hommes.
“Lengo la Mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wazazi ama walezi wa watoto
waliondolewa katika ajira na wale ambao walikuwepo katika dalili za
kuajiriwa… ili kuweza kuwapa mbinu za ujasiriamali jinsi ya kujitambua,
kubadirisha fikra, kuthubutu, kuanzisha biashara na kuzisimamia
kikamilifu bila uoga wowote ili kuweza kupata fedha za kuhudumia
familia zao bila matatizo yoyote,” alisema Komba na kuongeza:
Hivi vikundi vitakavyoundwa, watakuwa wanakutana na kuchangishana
mwenye uwezo wa sh 500 ama 1,000… wanachangisha na wanaweka katika
sanduku fedha zao na zikifikia sh 100,000 tutawakopesha laki tano na
zikifikia laki mbili tutawakopesha shilingi milioni moja na riba yake
ni asilimia 3 kwa miezi sita na mkopo huo utakuwa wa miezi mitatu hadi
sita.
Aidha, Komba alisema wamefanya hivyo ili kuwasaidia watoto waendelee
na masomo ambayo wamewadhamini, kwa sababu mtoto akitoka chuoni ama
shule, nyumbani kama hakuna mahitaji ya muhimu ya msingi atarudi
mtaani tena kuendelea na biashara yake ya kuajiriwa ama kujiajiri na
kujikuta anaingia katika ajira ya mapema.
“Ni lazima tuwapatie mkopo hawa wazazi, ili mwisho wa siku waweze
kuwasaidia watoto wao kuwanunulia mahitaji muhimu madogo madogo
akitoka chuoni ama shule ambako Fawopa tumewapeleka kusoma, akirudi
nyumbani akute mahitaji yote muhimu ya kibinadamu,” alisema.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Sharifa Ismail, Mkazi wa Kata
ya Reli na Salumu Ally, Mkazi wa Kata ya Vigaeni, waliishukuru Fawopa
kwa kuwapa mafunzo hayo ya ujasiriamali.
“Ki ukweli tunawashukuru Fawopa kwa kutupatia haya mafunzo na
wameahaidi kutupatia mikopo baada ya kumalizika kwa haya mafunzo,
kinachotakiwa sasa ni sisi wenyewe wazazi ama walezi kujitahidi kwa
moyo mmoja ili tuwe kitu kimoja tuweze kupata mikopo ambayo tutaweza
kuwasaidia watoto wetu,” walisema na kuongeza. Hili Shirika la Fawopa
ni watu wa kuigwa sana, yaani watawapeleka watoto wetu shule na chuo
kuwasomesha na sisi leo tunasaidiwa mikopo lazima tuowanyeshe moyo wa
dhadi kwao,” waliseama.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment