Home » » ALIYELETA HOFU ABAINIKA HANA EBOLA

ALIYELETA HOFU ABAINIKA HANA EBOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
KIJANA Ally Selemeni (30), mkazi wa Mikindani, mkoani Mtwara aliyeleta hofu kwa wananchi waliokuwepo katika maeneo ya hospitali ya Rufaa ya Ligula kuwa ana dalili za ugonjwa wa Ebola, anaendelea vema na imebainika hana ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hospitali hiyo, Selemani alisema kuwa alilazwa katika hospitali hiyo kutokana na kusumbuliwa na kifua kwa miezi miwili sasa.
Selemani aliyasema hayo kutokana na uvumi uliojitokeza mkoani humo kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola baada ya kutokwa na damu katika mwili wake kupitia puani na mdomoni kitendo kilichofanya wauguzi kumkimbia na kwenda kutafuta vifaa vya kujikinga na gonjwa huo.
“Watanzania wenzangu naomba wajue kuwa mimi sina ugonjwa wa ebola ila ni maneno ya watu tu baada ya kuona natoka damu katika mwili wangu wakajua nina huo ugonjwa,” alisema
Naye mdogo wa mgonjwa huyo, Sanjamin Abdallah (20) alisema kuwa kaka yake anasumbuliwa na kifua na sio kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola kama ilivyoelezwa na baadhi ya watu waliomuona.
Naye muuguzi aliyekuwepo zamu siku ya tukio, Mariam Mkanyama, alisema kuwa walipoona mgonjwa huyo anatokwa na damu puani na mdomoni walishitushwa na hali hiyo.
“Yaani tulipoona mgonjwa wa kifua anatoka damu puani na mdomoni tulipata na mshtuko mkubwa na tulikimbia kwenda kuchukua vifaa vya kujikinga zaidi kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo,” alisema.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu saa 4 asubuhi ikiwa ni siku ya tisa tangu mgonjwa huyu alazwe hospitalini hapo
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa