BARAZA
la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara limeitaka
halmashauri hiyo kuweka utaratibu kwa wafanyabiashara wilayani humo
kulipa kodi zao kwa njia za miamala ya kibenki ili kudhibiti mianya ya
rushwa na kuweza kukusanya mapato yake ya ndani kwa wingi zaidi.
Madiwani hao walitoa
mapendekezo hayo jana wakati walipokuwa wakichangia muhtasari wa kamati
ya kudumu ya uchumi kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani
lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo mijini hapa.
Walisema kuwa ili
kuweza kudhibiti mianya ya rushwa na kukusanya mapato mengi zaidi katika
halmashauri hiyo yanayotokana na kodi mbalimbali zinazolipwa na
wafanyabiashara ni
wakati mwafaka sasa kwa uongozi kuweka utaratibu wa kumtaka kila
mfanyabiashara kulipa kodi kwa kutumia njia za kibenki badala ya kulipa
kwa njia ya malipo keshi.
Walisema kwa utaratibu
wa sasa kwa wafanyabiashara kulipa kodi zao kwa kutumia malipo keshi
kupitia kwenye madirisha ya ofisi za fedha za halmashauri ni kuendelea
kuweka mianya ya rushwa na kuikosesha mapato halisi yanayotakiwa
kuyapata katika makusanyo yake ya ndani.
Kwa upande wake diwani
wa Kata ya Chanikanguo Samson Bushiri alisema iwapo wafanyabiashara
wilayani humo wakianza kulipa kodi benki mapato ya halmashauri
yatakusanywa kwa wepesi zaidi na kuondoa hali ya wasiwasi kwa madiwani
kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Alisema wao kama
madiwani wameingiwa na wasiwasi kuhusu utaratibu huo kwa wafanyabiashara
kulipa kodi zao kwenye ofisi za halmashauri kwani mara kadhaa
wameshuhudia kuwepo kwavitabu tofauti tofauti vinavyotumika kulipa kodi
kwa wafanyabiashara jambo ambalo linawapa wasiwasi madiwani hao juu ya
ukusanyaji wa mapato yake ya ndani.
“Kuanzia sasa
halmashauri iweke utaratibu wa kila mfanyabiashara kwenda kulipa kodi
zake benki kuliko kuendelea kulipa ndani ya ofisi hii itasaidia
kupunguza mianya ya rushwa na hata kuiwezesha kupata mapato yake ya
ndani kwa wingi zaidi,”alisema Bushiri.
Naye diwani wa Kata ya
Nanjota, Eduward Mmavele alisema utaratibu huo utasaidia kuifanya
halmashauri kupata mapato yake kwa wingi zaidi na kwamba utaratibu huo
ni wa usalama zaidi na ndio wa kisasa.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Beatrice Dominic alipongeza
mapendekezo hayo na kudai kuwa iwapo utaratibu huo ukiridhiwa na
madiwani utaanza kutekelezwa mara moja na kwamba kuanzia sasa wataanza
kuwahamasisha wafanyabiashara kwenda kulipa benki kodi zao.
“Kwa upande wangu hata
mimi naumia sana kichwa juu ya utaratibu wa wafanyabiashara kulipa kodi
zao hapa ofisini hivyo ninyi madiwani kama mmeliona hili basi itakuwa
vizuri kubadilisha utaratibu huu na sasa kila mfanyabiashara tutamueleza
akalipe benki,”alisema Dominic.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment