Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KIKUNDI cha Jipange cha kinamama wajasiriamali mkoani Mtwara,
wameilalamikia Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa, kwa kutowapa
sehemu ya kufanyia biashara zao licha ya kuwa wa kwanza kufika katika
eneo hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa uchungu maeneo ya
Bima wanapofanya baishara yao, Mwenyekiti Msaidizi wa kikundi hicho,
Amina Maulidi, alisema kuwa walifika eneo hilo la biashara kipindi
kirefu wakati pakiwa na pori.
“Hili eneo ni la CCM na tulipofika hapa tulilikuta chafu na hakuna
hata banda moja, baada ya sisi kuingia kama miaka sita mbele, wakaja
watu wa CCM kugawa viwanja kwenye eneo hili, lakini cha kushangaza sisi
akinamama wametukuta na wametuona lakini wametunyima kiwanja,” alisema
Amina na kuongeza.
Tulipeleka barua CCM Mkoa mwaka 2010 hatukupata majibu yoyote hadi
leo, wakati eneo hili tumesafisha, sisi tulikuta pana pori kweli, hapa
tulipo hatuna kiwanja wala hatuna eneo la kufanyia biashara ya
kudumu…eneo hili tunalofanyia biashara ni la huyu baba mwenye hii sheli,
baada ya kutuonea huruma tunahangaika ndipo alipotuambia tujenge hii
sehemu lakini tusijenge banda la kudumu kwa sababu wakati wowote anaweza
kutuambia anataka eneo lake.
Hata hivyo, Amina alisema kuwa kama mwenye eneo akilitaka, watakuwa
hawana tena sehemu ya kufanyia biashara yao na ikishindikana kabisa,
watakwenda kupanga biashara yao mbele ya ofisi ya CCM Mkoa au ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, kwa sababu biashara hiyo ndiyo inayowaendeshea maisha yao
ikiwemo kulipa kodi ya nyumba pamoja na kusomesha watoto wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho, Asha Kumpeta, alisema
kuwa kikundi chao kilianza biashara mwaka 2000 katika eneo hilo la CCM
na walilikuta eneo hilo likiwa chafu, wakawa wanalima wanaweka meza
chini ya mwembe wanapanga bidhaa zao.
“Sisi tulishaandika barua na kupeleka CCM Mkoa, lakini baada ya miezi
kama nane au tisa walikuja kugawa viwanja sisi tulikosa, tukaenda tena
kwa katibu wa CCM kufuatilia na tulipowauliza kwa nini tumekosa kiwanja,
walitujibu subirini kuna eneo limebaki kama maeneo tatu hivi
tutawapatia,” alisema Kumpeta na kuongeza:
Lakini baada ya kuona kimya, tulienda tena wakatuambia lile eneo
limeshachukuliwa, kiukweli tuliumia sana ila hatukuwa na jinsi…Ombi letu
sisi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia,
atakoposikia kilio chetu tunaomba atusaidie sisi akinamama eneo la
kufanyia biashara na liwe la kwetu na la kudumu, kwani uwezo wa kujenga
wenyewe tunao kinachotakiwa tupatiwe tu eneo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment