Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ABIRIA wanaotumia barabara itokayo Mtwara kwenda Tandahimba na
Newala wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuitengeneza kwa kiwango
cha lami licha ya kusafirisha korosho wakati wa mavuno.
Akizungumza na Tanzania Daima, Halima Saidi mkazi wa Kijiji
cha Mtama, wilayani Tandahimba, alisema barabara hiyo imekuwa kero
kwao hata hivyo wanaiomba serikali kuifanyia kazi haraka kwa vile ndiyo
tegemeo kwa wakulima wa korosho zao linaloingiza fedha kwenye pato la
taifa.
“Barabara ya Tandahimba-Newala tumesahaulika, hii barabara sio ya
kuwa na vumbi na makorongo hadi leo hii wakati serikali inapata fedha
nyingi kutokana na korosho kipindi cha msimu kwani hata magari
yanayosafirisha korosho ni mengi yanalipia ushuru,” alisema Halima.
Alisema ni aibu kwa viongozi wa kusini mpaka leo kuwa kimya bila
kupigania barabara zikajengwa kwa lami ili kumsaidia msafiri kufika kwa
wakati aendako na kuondoa kero ya usafiri wakati wa mvua.
“Wilaya ya Tandahimba ina mapato mengi kupitia korosho lakini haina
barabara ya lami… aibu kwa halmashauri tangu nizaliwe miaka 56
iliyopita nimeikuta barabara ina vumbi mpaka leo haijawekwa lami.
“Unasafiri kutoka Tandahimba ama Newala hadi mtu ufike Mtwara unakuwa
kama kinyago kwa sababu ya vumbi… kwanini wasiige Mbeya na
Kilimanjaro?” alisema Halima.
Hassani Chikota mwanakijiji wa Mkwiti, wilayani humo alisema barabara
hiyo kwa sasa inaonekana safi haina mashimo kwa sababu mwenge wa
uhuru umepita ndio maana unaona wamechonga barabara.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment