SERIKALI
ya Tanzania inatarajia kutuma wataalam kwenda nchini Canada katika
Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya jimbo la British Columbia (BC Oil&
Gas Commission) ili kupata uelewa zaidi katika masuala ya udhibiti wa
mafuta na gesi nchini.
Hayo yalisemwa na Naibu
Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga
wakati akizungumza na watendaji wa Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya Jimbo
la British Columbia katika Ofisi za kamisheni hiyo zilizo katika mji wa
Victoria nchini Canada.
Akiongoza ujumbe wa
Tanzania uliotembelea kamisheni hiyo ili kujifunza masuala ya udhibiti
wa sekta ndogo ya gesi asilia na mafuta, Naibu Waziri alisema kuwa lengo
la Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo
zinaendelezwa na faida yake kuonekana kwa wananchi hivyo wataalam
watakwenda nchini Canada katika kamisheni hiyo ili kuongeza uelewa
katika masuala ya udhibiti ambao kwa kiasi kikubwa unachangia katika
kuhakikisha kuwa na maendeleo endelevu ya rasilimali zilizopo Tanzania.
“Mtazamo wa wananchi
wengi ni kuwa makampuni ya kigeni yanakuja nchini Tanzania kuchukua
rasilimali na kuondoka nazo bila wananchi hao kufaidika hivyo serikali
inafanya kila jitihada ili faida za rasilimali zetu ziwafikie wananchi
wote na moja ya vigezo vya jitihada hizo ni kuwa na mamlaka madhubuti za
udhibiti zitakazo hakikisha makampuni ya nje na ndani ya nchi yanafanya
kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria zinazoongoza sekta husika,”
alisema Kitwanga.
Naibu Waziri alieleza
kuwa Tanzania ikiwa katika mchakato wa kutengeneza sheria na kanuni
zitakazoongoza sekta ya gesi asilia na mafuta, inahitaji kupata maoni na
uelewa zaidi kutoka katika nchi zilizopiga hatua katika uendelezaji wa
rasilimali hizo ikiwemo jimbo la British Columbia ambalo limegundua gesi
asilia kiasi cha zaidi ya futi za ujazo trilioni 2,900.
Naye Ofisa Mkuu wa
Operesheni katika Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya British Columbia,
Mhandisi Ken Paulson alieleza kuwa kamisheni hiyo ambayo imeanzishwa
zaidi ya miaka 15 iliyopita ina jukumu la kudhibiti shughuli zote za
mafuta na gesi asilia ikihusisha, utafiti, uendelezaji na usafirishaji
wa rasilimali hizo kwa njia ya bomba.
Mhandisi Paulson
alieleza kuwa kamisheni hiyo pia ina jukumu la kukusanya takwimu za ki
jiolojia zinazotumika katika shughuli za utafutaji wa gesi asilia na
mafuta na kuzitangaza kwa njia ya tenda ili makampuni yanayohitaji
kufanya shughuli za utafutaji mafuta na gesi katika jimbo hilo yanunue
takwimu hizo kutoka kamisheni hiyo.
Kuhusu matumizi ya gesi
asilia, Ofisa Mkuu wa Operesheni aliueleza ujumbe huo kutoka Tanzania
kuwa asilimia 15 ya kiasi cha gesi kilichogunduliwa katika jimbo hilo
kinatumika ndani ya jimbo la British Columbia kwa matumizi mbalimbali na
kiasi kinachobaki kinasafirishwa kwenda bara la Amerika Kaskazini.
Kuhusu mfumo wa
ugawanaji mapato (PSA) kati ya kampuni ya utafutaji na uchimbaji gesi
asilia na mafuta, Mhandisi Paulson alieleza kuwa kampuni ikianza
uzalishaji wa gesi au mafuta, serikali ya jimbo hilo hukusanya mrabaha
wa asilimia 10 hadi 20 ya mapato.
Katika ziara hiyo ya
mafunzo nchini Canada, Naibu Waziri wa Nishati na Madini ameambatana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo, Murtaza
Mangungu, Raya Ibrahim, Richard Ndasa, Deogratias Ntukamazina, Shafin
Sumar na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment