Home » » MEWATA YAOMBWA KUONGEZA NGUVU UPIMAJI SARATANI VIJIJINI

MEWATA YAOMBWA KUONGEZA NGUVU UPIMAJI SARATANI VIJIJINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Chama cha Madaktari Wanawake (Mewata) kimeombwa kuongeza nguvu kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa kansa ya titi kwa wanawake wa vijijini.
Ombi hilo lilitolewa jana na mkazi wa Nanyamba, wilaya ya Mtwara, Rukia Mpandu (60), ambaye alipata tatizo hilo mwaka jana na kushindwa kuhudhuria zoezi la upimaji wa kansa uliofanyika Desemba mwaka jana, katika Shule ya Msingi Magomeni, mjini Mtwara.
Akizungumza na NIPASHE mjini hapa jana, Rukia alisema madaktari hao wanatakiwa kujikita zaidi vijijini ili kuwasaidia wanawake wasio na uwezo kupata huduma hiyo mapema badala ya kwenda hospitali za mikoa.

Rukia ambaye ni mlemavu wa miguu amelazwa wodi ya wanawake  namba moja, alisema alishindwa kuhudhuria upimaji huo baada ya kukosa nauli ya Sh. 3,500 ya kwenda Nanyamba kuhudhuria uchuguzi uliokuwa unafanywa  bure na Mewata mjini hapo.

 “Wakati madaktari wamefika Mtwara mjini ndiyo nilikuwa nahisi maumivu  katika titi  langu la mkono wa kushoto, lakini kutokana na hali yangu ya ulemavu sina kazi yoyote ya kuniingizia pesa nilishindwa kufika hapa.”

“Naishi na mume wangu ambaye pia ni mlemavu wa miguu, madaktari walipofika nilikuwa ndiyo naanza kusikia  maumivu makali, nilikuwa  sijapata hata kidonda kama ilivyo sasa, hali hii imejitokeza baada ya kukosa  uchunguzi  mapema, kama ningefanikiwa kufika na kufanyiwa uchunguzi hali yangu  isingefikia hapa.” alisema kwa masikitiko mama huyo.

Alisema umasikini uliokithiri katika jamii umekuwa ukichangia kuleta madhara makubwa miongoni mwa jamii, na kuleta athari ambazo zingeweza kuzuilika.

“Nauli ya kunifikisha hapa Ligula nimechukua fedha ya Tasaf ambayo nilipewa kwa ajili ya kununua chakula, lakini nimelamizika kuacha kununua chakula baada ya afya yangu kuwa mbaya” aliongeza kusema.

AOMBA MSAADA

Mpandu, ambaye amelazwa hospitalini hapo kwa takribani siku 18 sasa, amepata rufaa ya kwenda kupata matibabu zaidi katika Taasisi ya Kansa Ocean Road jijini Dar es Salaam.

“Nimepata rufaa ya kwenda kutibiwa Dar es Salaam, nimeambiwa nitatibiwa bure, lakini wameniambia kuwa lazima niwe na Sh. 20,000 kwa ajili ya kumsaidia nitakayeondoka naye hapa kwa ajili ya kunihudumia huko.”

 “Sina kazi nimeshindwa kupata kiasi hiki mpaka sasa, hivyo nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie  na watu wenye mapenzi  mema wanisaidie ili niweze kupata matibabu” alisema huku akibubujikwa machozi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa