Home » » WALIOUA MTWARA DAR WAKAMATWA

WALIOUA MTWARA DAR WAKAMATWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kukamata majambazi wanane kati yao, wawili wanahusishwa moja kwa moja na tukio la mauaji ya Mtawa wa Kanisa Katoliki, marehemu Clesencia Kapuri (50), na kumpora sh. milioni 20 Juni 23 mwaka huu, Ubungo Kibangu.

Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Aliwataja majambazi wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Manase Ongenyeka (35) kwa jina maarufu ‘Mjeshi’, mkazi wa Tabata Chang’ombe ambaye pia ni mwendesha pikipiki ya bodaboda na Hamisi Ismail au Carlos ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Magomeni, wote wakazi wa Dar es Salaam,

“Majambazi hawa licha ya kuhusishwa na tukio la mauaji ya Mtawa ni watu hatari waliokuwa wakitafutwa muda mrefu kwa tuhuma za kuhusika na uporaji kwenye Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni Aprili 15 mwaka huu, wakitumia pikipiki.

“Huyu Manase ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki akiwa amewabeba wenzake Carlos na mwingine anaitwa Hamis Ismail... Carlos ndiye alikuwa kiongozi katika tukio hilo,” alisema Kamishna Kova.

Aliongeza kuwa, jeshi hilo linaendelea kuwatafuta majambazi wengine wawili ambao walihusika katika tukio la mauaji ya Mtawa na jambazi mmoja aliyehusika kwenye tukio la uporaji Barclays.

“Hawa majambazi wote tuliowakamata, wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya ujambazi jijini Dar es Salaam wakitumia silaha za moto ambazo ni bunduki aina ya SMG, bastola na vifaa vya uvunjaji,” alisema.

Aliwataja majambazi wengine waliokamatwa kuwa ni Beda Mallya (37), ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Msakuzi, Michael Mushi au Masawe (50), mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makabe-Kimara na Sadick Kisia (32), mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Kizuiani.

Wengine ni Elibariki Makumba (30) na Nurdini Suleiman (40), wote wakazi wa Buguruni Madenge na Mrumi Salehe au Chai Bora (38), mkazi wa Kigogo Fresh.

Kamishna Kova alisema, majambazi watatu Makumba, Suleiman na Mrumi, walikamatwa baada ya kutumia mbinu ya hati bandia kutaka kuomba kazi kwenye makampuni binafsi ya ulinzi iitwayo Instant Security Services, iliyopo Mtaa wa Msasani Makangira.

Majambazi hao walitaka kazi hiyo ili baadaye waweze kufanya uhalifu au kuuruhusu mtandao wao uweze kutenda uhalifu; hivyo aliyahadharisha makampuni binafsi ya ulinzi, kuwa makini na ajira wanazotoa kutokana na majambazi wengi kwenda kuomba kazi katika makampuni yao.

“Tunawashauri wanapotaka kuajiri, washirikiane na Jeshi la Polisi ili waweze kufanya upekuzi wa pamoja ambao utahusisha alama za vidole, picha na ukaguzi wa kumbukumbu muhimu za kibayologia kama vipimo vya DNA na vingine,” alisema Kamishna Kova.

Aliongeza kuwa, upelelezi wa mashauri mbalimbali yanayowahusu majambazi hao unaendelea na hatimaye majalada ya kesi yatapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kabla ya kupelekwa mahakamani

 chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa