Home » » AFA BAADA YA KUTIMULIWA UANACHAMA WA USHIRIKA

AFA BAADA YA KUTIMULIWA UANACHAMA WA USHIRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Zao la Korosho wa Wilaya za Tandahimba na Newala (Tanecu), mkoani Mtwara, Shaibu Namkuna, amefariki dunia, baada ya kufukuzwa uanachama kwa tuhuma za kushawishi wanachama kuugawa ushirika huo.
Namkuna alikuwa ni mmoja wa wajumbe wanne, wakiwamo madiwani wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliofukuzwa uanachama kwa tuhuma hizo.

Walichukuliwa hatua hiyo  katika Mkutano Mkuu wa Tanecu, uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 200, wilayani Newala, mwishoni mwa wiki iliyopita.Wanatuhumiwa kuchochea mgawanyiko katika chama hicho wakitaka kila wilaya ijitegemee.

Tuhuma hizo zilifikishwa mezani kwa Mwenyekiti wa Tanecu, Yusufu Nannila, ambaye alikuwa akiendesha mkutano huo.

Wajumbe wa mkutano huo hawakufurahishwa na tuhuma hizo, hivyo kwa kauli moja wakapitisha azimio la kutaka watu hao wafukuzwe uanachama.

Baada ya wajumbe hao kufukuzwa uanachama na kutoka nje ya ukumbi, Namkuna alipatwa na shinikizo la damu.
Hali hiyo ilimfanya akimbizwe Hospitali ya Wilaya ya Newala, ambako mauti yaliyomkuta.

Siku 21 kabla ya kukutwa na mauti, Namkuna aliiandikia Tanecu barua akiitaka igawanywe ili kila wilaya iwe na chama chake badala ya ilivyo, kwa madai kwamba, chama hicho hakiwasaidii wakulima, bali kipo kwa kuwanufaisha viongozi wake.

Mjumbe mwingine, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Miminche kutoka Wilaya ya Tandahimba, Hamadi Mnene, alisema kabla ya Mkutano Mkuu alifuatwa na watu wanne, wakiwamo madiwani wawili wa CCM kutoka wilayani humo,    wakitaka akubali kuunga mkono hoja yao ya kuugawa ushirika.Hata hivyo, alisema baada ya kukataa hoja hiyo, walianza kumtishia.

Alisema jambo hilo lilimfanya kuhama nyumbani kwake kwa wiki moja.Katika mkutano huo, Ulenje alituhumiwa kufanya mikutano ya uchochezi kuwashawishi wajumbe kukubali ajenda ya kuigawa Tanecu mkutanoni.

Mwenyekiti wa mkutano huo alitoa nafasi kwa watu hao kujieleza mbele ya wajumbe.Wote walikiri kufanya hivyo na kuuomba mkutano uwasamehe. Hata hivyo, wajumbe walikataa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa