Home » » Watanzania watangaziwa kununua hisa, kuwekeza kwenye mafuta, gesi

Watanzania watangaziwa kununua hisa, kuwekeza kwenye mafuta, gesi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Swala (Tanzania) PLC, Dkt. David Mestres Ridge (Watatu kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Abdullah Mwinyi (Wapili kushoto), mkurugenzi mtendaji mwenza, Selemani Pongoloni (Kulia) na Mkurugenzi Mshauri wa kampuni Lyen Jay Nsemwa, wakionyesha Muhtasari wa hatua mbalimbali ambazo kampuni hiyo imefikia katika utafutaji mafuta na gesi hapa nchini, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kampuni hiyo imetangaza ufunguzi wa ofa yake ya awali kwa umma ijulikanayo kwa kifupi (IPO), yenye hisa za kawaida milioni 9.6 ambapo itauza hisa hizo kila moja kwa Shilingi mia tano (500),kuanzia jana Juni 9. Picha na Khalfan Said
Wakati zoezi la kuomba vibali kwa ajili ya kutafuta vitalu likiendelea kutangazwa na serikali kwa kampuni zenye uwezo wa kumudu gharama za utafutaji huo, Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Swala Tanzania PLC, imewatangazia Watanzania kuanza kununua hisa kwenye kampuni hiyo za kuwekeza kwenye rasilimali ya mafuta.
Kampuni hiyo ambayo Watanzania wanaoumiliki wa asilimia 35 na Australia asilimia 65, ilitangaza ufunguzi wa ofa yake ya awali kwa umma inayojulikana kwa jina la IPO yenye hisa za kawaida 9, 600, 000, jana jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo nchini, Abdullah Mwinyi, alisema kampuni hiyo ambayo  ni ya kwanza nchini kushirikisha kuuza hisa katika soko la hisa,  dhamira yao ni kumiliki hisa hizo kwa asilimia 35.

Kwa mujibu wa Mwinyi, kampuni hiyo itakuwa ikiuza kila hisa kwa Sh. 500 kuanzia jana hadi Julai 4, mwaka huu na kwamba kutolewa kwa tangazo hilo kumekuja ikiwa ni wiki moja baada ya wao kupokea rasmi idhini kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) na kuifanya kuwa ofa ya kwanza kufanyika kwenye sekta ya gesi na mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema fomu za maombi na nakala ya waraka wa matarajio zitakuwa zinapatikana katika ofisi za mawakala wenye leseni kutoka soko la hisa la Dar es Salaam (DSE), katika matawi ya benki ya CRDB na ofisi za Arch Financial & Investment Advisory Ltd na kwamba hakuna ukomo wa kununua hisa hizo huku kiwango cha chini kikiwa ni hisa 100.

Mkurugenzi Mtendaji wa Swala, David Mestres Ridge, alisema kuzinduliwa kwa ofa hiyo ni hatua kubwa siyo tu kwa ajili ya  kampuni hiyo, lakini pia ni kwa ajili ya Watanzania wote na kwamba kuwekeza hisa katika mafuta na gesi ni moja ya njia za kupanua wigo wa kiuchumi kwa mtu yeyote kwani inaruhusu yeyote kumiliki hisa katika biashara hiyo inayokua kwa kasi.

Lengo lingine ni kuona Watanzania wanakuwa na umiliki wa rasilimali zao huku akiishukuru serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli  (TPDC) na  CMSA kwa kuwaruhusu kuwa kampuni ya kwanza ya mafuta na gesi katika Afrika Mashariki na kumilikiwa na umma.

Naye mshauri katika kampuni hiyo, Basil Mramba, aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kununua hisa hizo kwa bei hiyo ya chini kwani baada ya kazi ya utafutaji ikimalizika na uvunaji kuanza, gharama za kununua zinakuwa kubwa.

Kampuni hiyo hujishughulisha na utafutaji wa mafuta na gesi katika mfumo wa bonde la ufa la Afrika Mashariki ikiwa na umiliki wa hisa wa asilimia 50 na ikiwa na leseni ya uendeshaji wa maeneo ya Kilosa-Kilombero na Pangani kwa kuhusisha hadi maeneo ya Same, Kilimanjaro.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa