Home » » NDANDA FC KUANZA KUJIFUA JUMATATU

NDANDA FC KUANZA KUJIFUA JUMATATU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

TIMU ya Ndanda FC yenye maskani yake Kijiji cha Njenga, Kata ya Mwena, Tarafa ya Chikundi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, inatarajiwa kuingia kambini Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Katibu Mtendaji wa Ndanda FC, Selemani Kachele, alisema kuwa wachezaji wote wanatarajiwa kufika Mtwara kesho kwa ajili ya kuingia kambini na Juni 9 wataanza rasmi mazoezi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
“Kambi ya wachezaji itakuwa hapa hapa Mtwara Mjini na wachezaji wote wa Ndanda FC wanatakiwa kufika Mtwara Mjini Jumapili ya tarehe 8 na tarehe 9 wataanza rasmi mazoezi katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona kabla hawajaanza ukarabati, na watakapoanza tutakwenda sehemu nyingine kufanyia mazoezi yetu,”  alisema Kachele.
Hata hivyo, Kachele alisema kuwa watakaa kambini wiki moja kisha watafanya ziara kwenye wilaya mbalimbali ili kucheza na kombaini za huko na kuangalia vipaji pia.
“Tutakaa wiki moja hapa Mtwara Mjini, halafu tutafanya ziara kwenye wilaya mbalimbali kama Manispaa ya Mtwara/Mikindani, Mtwara Vijijini, Newala, Tandahimba, Nanyumbu na Masasi, tutaenda kucheza na timu za kombaini na humo walimu watapata fursa vile vile ya kuangalia vipaji vya huko, ambao wataweza kusaidia kujenga timu yetu kama si kwenye timu A hata kwenye timu B vile vile, kwa sababu kwa mujibu wa TFF tunakuwa na timu A na B,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa