Home » » STAKABADHI GHALANI KITANZINI CHA WAKULIMA-2

STAKABADHI GHALANI KITANZINI CHA WAKULIMA-2

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkulima wa Korosho katika kijiji cha Makonga wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, Rehema Bakari akiwa amesimama nje ya nyumba yake akiwa na watoto wake waliokaa, Amina Bakari (kulia) na Fatuma Bakari (kushoto). Picha:Gwamaka Alipipi
Katika toleo la jana tulielezea karaha mbalimbali kuhusiana na mfumo wa stakabadhi ghalani unavyowasababishia umaskini wakulima wa korosho Kusini mwa Tanzania.
Sehemu ya pili ya makala hii inaelezea mambo mbalimbali kuhusiana na mfumo huo ikiwamo kushuka kwa uuzaji wa korosho.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Umoja kilichopo wilayani Liwale, Hassan Myao, anathibitisha kuwa wakulima wa korosho hawakulipwa malipo kwa msimu wa 2012/13, sababu ikielezwa kuwa ni kushuka kwa bei ya korosho kwenye soko la dunia.

Anasema kutokana na hali hiyo, waliuza tani 800 za korosho kwa bei ya Sh. 1,150 kwa kilo. Tani moja ni sawa kilo 1,000.Anasema kwa upande mwingine, stakabadhi ghalani imechangia hali hiyo, hivyo kuhusishwa na ghasia zilizotokea mwaka jana na kusababisha uharibifu wa mali.

 Mwenyekiti wa chama cha msingi katika kijiji cha Mbuli, Abubakar Hamza, anasema katika miaka ya 2000, kijiji hicho kilikuwa kinazalisha korosho hadi kufikia tani 200.

Anasema katika kipindi cha mwaka jana, walizalisha tani 74 kutokana na wakulima wa korosho kukata tamaa, kuachana na zao hilo, badala yake kujishughulisha na mazao mengine.

Ofisa Kilimo Msaidizi katika wilaya ya Tunduru, Fidelis Nyakunga, anathibitisha kuchelewa kwa malipo ya pili ya korosho hususani kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011, akisema hali hiyo inasababishwa na ufanisi duni wa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Anatoa mfano kuwa, kipindi hicho (2011), bei ilikuwa Sh. 850 kwa kilo, hivyo ikasababisha chama cha ushirika cha Amcos wilayani Tunduru, kukosa fedha za kurejesha mkopo wa benki uliochukuliwa kwa malipo ya awali.

Hata hivyo, stakabadhi ghalani ilisitishwa wilayani Tunduru tangu mwaka 2012 na sasa wakulima wanauza korosho zao kwa kutumia mfumo wa soko huria.

VURUGU ZAHUSISHWA NA KOROSHO
Vurugu zilizotokea mwaka jana wilayani Liwale zikisababishwa na wakulima wa korosho kutolipwa malipo ya pili kwa wakati, zimewafanya miongoni mwao kubadili aina ya mazao kutoka kwenye korosho na kulima ufuta.

Vurugu hizo zilisababisha mali kama vile magari na nyumba za taasisi na raia wakiwamo viongozi na wawakilishi wa umma kuharibiwa.Matukio hayo yalijumuisha kuchoma moto nyumba za viongozi waandamizi, makao makuu ya halmashauri ya wilaya na maghala ya mazao.

 Nyumba zilizochomwa moto ni za Mbunge wa Liwale (CCM), Faith Mtambo, Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Umoja, Hassan Myao na Makamu wake, Hassan Mpako na Diwani kupitia viti maalumu (CCM) Liwale, Amina Mnocha.

Pia zilikuwapo za Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas Chigogola ambaye pia ng’ombe wake tisa walikatwa kwa mapanga hadi kufa, wakiacha ndama watatu.

Nyingine ni nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Liwale, Mohamed Ng’omambo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Lindi, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Minali, Mohamed Limbwilindi na Katibu wa chama hicho, Juma Majivuno.

HUDUMA DUNI
Hali ngumu ya maisha inayotokana na ukosefu wa huduma bora za jamii, haipo kwa mkulima mmoja mmoja wa korosho katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania, bali na jumuiya za wakulima.

Mathalani, wakazi wa kijiji cha Malamba wilayani Tandahimba, katika kujikwamua na hali ngumu ya upatikanaji wa maji kijijini hapo, wameamua kuchimba bwawa maarufu kama ‘lambo’.

Pia, vipo visima vidogo vilivyochimbwa kwenye eneo linaloitwa theruji. Asili ya jina hilo (theruji) haikujulikana.

KUSITISHWA KWA UUZAJI HURIA
Hatua ya kusitisha uuzaji korosho kwa mfumo huria, uliingia dosari katika maeneo mengi ya Kusini mwa nchi, baada ya stakabadhi ghalani kuthibitika si ‘mwarobaini’ wa kumuinua mkulima kiuchumi.

Abilahi Mohamedi ni mkulima katika kijiji cha Mwindi wilaya ya Tandahimba, anasema usitishwaji huo uliofanyika Oktoba, 16, 2011 ulisababisha mgogoro kati ya serikali mkoani Mtwara na wakulima wa korosho.

UONGEZAJI THAMANI YA KOROSHO
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mgomi, anasema ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, serikali itakuwa katika hatua ya mwisho ya ujenga viwanda vya kubangulia korosho katika vijiji vya Mnavile, Nanjota na Mkululu mkoani Mtwara.

Anasema kwa sasa kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha kutoka kwa wafadhili (hakuwataja) ili kuanza kwa ujenzi wa viwanda hivyo.
Kwa mujibu wa Mgomi, viwanda hivyo vitachochea uboreshaji wa kilimo cha korosho kwa kuliongezea thamani zao hilo.

STAKABADHI GHALANI UNAFAA WAKUBWA
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Andrew Kalinga, anasema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri kwa wakulima wakubwa na kwamba haufai kwa mkulima wa kipato cha chini.

“Mfumo uwapo, lakini usimlazimishe mkulima kuutumia. Pia mfumo huu ungesimamiwa vizuri ungeleta manufaa mazuri kwa mkulima,” anasema.

SHERIA ILIYOPO
Zao la korosho linaongozwa kwa sheria mpya ya korosho namba 18 ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2010.Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT), Mfaume Juma, anasema ‘chombo’ hicho kimepewa jukumu la kusimamia shughuli zinazohusu zao hilo katika uzalishaji, ubanguaji, masoko na utafiti.

Anasema hali hiyo inalenga kuhakikisha kuwa korosho inatoa mchango wake katika maendeleo ya wakulima na taifa kwa ujumla.
“Hivyo katika muktadha huo wakulima wa korosho wanapokuwa na madai ya kutolipwa fedha zao kwa kipindi kirefu, kazi ya Bodi ni kufuatilia ili kuhakikisha kuwa wanapata malipo yao bila kuathiri ufanisi wa sheria zingine zinazosimamia biashara ya korosho,” anasema.

Anasema Bodi kwa kushirikiana na wasimamizi wengine inaendelea na kazi ya kuwaelimisha wakulima kuhusu sheria hizo ambazo wakulima hawana uelewa nazo.

Anasema upo uwezekano kwa mujibu wa Sheria ya Stakabadhi Mazao Ghalani na ile ya Ushirika ya mwaka 2013 kuwachukulia hatua watakaobainika kuwadhulumu wakulima wa korosho malipo ya pili.

UKUBWA WA GHARAMA
Mbali na athari zinazotokana na stakabadhi ghalani, imebainika kuwa mabadiliko katika mfumo wa soko la kimataifa, yamechangia kufifisha uzalishaji wa korosho na kuleta umaskini miongoni mwa wakulima.

Hilo limebainika kupitia tafiti zilizowahi kufanywa na taasisi mbalimbali kuhusu zao la korosho ikiwamo Agricultural Non State Actors Forum (Ansaf).

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Ansaf na kutolewa mwaka jana, unaonyesha kuwa wakulima wa korosho katika mikoa ya kusini mwa Tanzania wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo ucheleweshwaji wa upatikanaji wa pembejeo kwa wakati.

Baadhi ya vijiji katika wilaya ya Tunduru mkoani Mtwara, mathalani Azimio na Kitanda, hakuna maduka ya pembejeo, hivyo husababisha wakulima kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani kuzinunua.

Wanasema hali hiyo inachangia ongezeko la gharama, hivyo huwafanya washindwe kuzitumia hasa dawa za kuua wadudu wanaoathiri korosho.Baadhi ya vijiji vipo takribani umbali ya kilometa 30 kutoka maeneo ya mijini. Usafiri wanaotumia ni pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ na wanatozwa kiasi cha kati ya Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa safari moja.

Inaelezwa kuwa gharama ya dawa ya Sulphur ya unga yenye ujazo wa kilo 25 ni Sh. 45,000, ikielezwa kuwa ni kubwa kiasi cha kuwafanya wakulima wengi washindwe kuinunua.

Yusuph Ause ni mkulima wa korosho katika kijiji cha Kitanda mwenye familia ya watoto tisa, anasema sababu kubwa inayosababisha korosho kushambuliwa na magonjwa kama bilihunga na mkausho wa majani kiasi cha kuathiri uzalishaji, ni ucheleweshwaji wa pembejeo.

Anasema dawa za kupulizia zinawafikia pasipo mpangilio wa muda mahususi, licha ya kwamba hata bei zake ni ghali hivyo wakulima wengi wanashindwa kuzimudu.

HUDUMA DUNI ZA JAMII
Huduma za kijamii katika maeneo mengi yenye makazi ya wakulima wa korosho, zipo katika hali duni ikilinganishwa na pato linalozalishwa kutokana na kilimo cha zao hilo na maeneo mengine hazipo kabisa.

Kwa mfano, upatikanaji maji katika kijiji cha Kitanda ni wa shida hali inayowalazimu kutembea umbali wa maili 15 kuyafuata katika eneo la Makondeko au Mitema.

Kadhalika hata maeneo hayo pindi maji yanapokauka, wakulima wa vijiji vya karibu wanalazimika kununua kwa Sh. 300 katika ujazo wa lita 20.
Kwa upande wa afya, kijiji cha Makonga kina wauguzi wawili wanaofanya kazi katika zahanati iliyopo eneo hilo.

Hata hivyo, ni jambo la kawaida kwa zahanati hiyo kufungwa kwa kipindi cha kuzidi mwezi mmoja, kutokana na likizo ama kusafiri kwa wauguzi hao.

Hali ya kufungwa kwa zahanati hiyo ikitokea, wanakijiji wa Makonga huwalazimu kwenda hospitali ya wilaya Newala, kwa kutumia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wakitozwa nauli ya Sh. 5,000, ikilinganishwa na usafiri wa basi unaogharimu Sh. 1,000.

BODI YA KOROSHO YATHIBITISHA
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT), Mfaume Mkanachapa Juma, anakiri kuwapo kwa ucheleweshwaji wa pembejeo na kusema: “Miaka ya 2000 kulikuwa na ucheleweshaji wa pembejeo, lakini kwa sasa hali hiyo imesharekebishwa.”

Anasema hadi kufikia Aprili 31, mwaka huu pembejeo zilizoagizwa zilikuwa zimewafikia wakulima kinyume cha ilivyokuwa takribani miaka miwili iliyopita.

Anasema pembejeo hizo zinapofika, zinathibitishwa na CBT ili kuzibaini kama zina ubora unaotakiwa, hiyo ikiwa ni moja ya njia za udhibiti wa pembejeo bandia.

URASIMU WA KUAGIZA PEMBEJEO
 Mfumo wa usambazaji pembejeo umekua tishio kubwa kwa zao la korosho nchini, wengi wa wakulima wamekuwa wakilalamika kutopata pembejeo kwa wakati.

Kadhalika, uchelekeshwaji huo wa pembejeo unasababisha mikorosho kutotoa korosho nyingi na kusababisha uzalishaji mdogo.

Mmoja wapo wa mkulima aliyekumbwa na hali hiyo ni Madai Salumu, mkazi wa kijiji cha Mtunguru wilaya ya Newala, anasema kwa mwaka juzi, ilimchukua miezi mitano kupata mifuko sita ya dawa ya maji aina ya SUBA chlor 48EC inayotibu mbu wa mikorosho.

“Pembejeo zinaletwa muda usiokuwa muafaka, kwa mfano mkulima akiagiza mifuko sita ya pembejeo, anapatiwa miwili,” anasema.
 

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja wilayani Liwale, Hassan Myao, anasema Ushirika haupaswi kuhusishwa moja kwa moja na ucheleweshwaji wa pembejeo.

Anasema kwa mujibu wa kanuni za utendaji, Ushirika unaandika barua kwa Mwenyekiti wa mfuko wa pembejeo wa wilaya ambaye ni Mkuu wa wilaya.
Anasema Mkuu wa wilaya  anawajibika kuitisha kikao cha kamati ya mfuko wa pembejeo wa wilaya ili kupitisha mahitaji.

“Pembejeo zinapowasilishwa wilayani, wakuu wa vyama vya msingi wanakwenda kuchukua na kuwagawia wakulima,” anasema.

Hata hivyo, anasema ucheleweshwaji wa pembejeo unaanzia ngazi ya mkoa ambapo inachukua takribani miezi mitatu kuzifikisha wilayani.
NIPASHE imebaini kuwa mkulima anahitaji kupulizia mikorosho Aprili inapotoa maua, lakini anaathiriwa na ucheleweshaji wa pembejeo zinazomfikia Julai.

Inaelezwa kuwa mikorosho mingi wilayani Newala imeshindwa kutoa mazao kwa wingi, kutokana na kukosa dawa ya kupulizia katika miezi ya Aprili hadi Juni, kipindi ambacho pembejeo zinakuwa hazijafika vijijini.

DAWA BANDIA
Uwapo wa dawa bandia umebainika kuwa miongoni mwa vyanzo vinavyoathiri kilimo cha korosho.Hali hiyo inadhihirika katika maeneo ya Newala, Masasi, Liwale, Tunduru na Tambahimba.

Athari za dawa hizo zilithibitika katika kijiji cha Malamba ambapo msimu wa 2012/13, wakulima waliuziwa dawa bandia aina ya MOVL iliyosababisha ukaukaji wa maua ya korosho kwa haraka.

Kutokana na hali hiyo, wakulima wengi waliathirika kwa mikorosho yao ‘kuungua’ hivyo kupata mavuno hafifu yaliyowaingia mapato kidogo.Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Malamba wilayani Tandahimba, Rashidi Mpanje, anathibitisha kuwapo kwa dawa hiyo.

Anasema ilipouzwa mara ya kwanza, wakulima walielekezwa kuwa vipimo vyake ni mililita 10 kwenye ujazo wa maji ya lita moja, matumizi ambayo yalisababisha kukauka kwa maua ya mikorosho.

Anatoa mfano wa athari za dawa bandia hiyo kuwa ni alivyopata mavuno ya kilo 27 kwa msimu huo, ikilinganishwa na kilo 880 alizozivuna msimu wa 2011/12.

Mpanje ana watoto watatu, wawili wanasoma shule ya msingi Malamba na mmoja anasoma shule ya sekondari Namikupa.Wote hao walishindwa kuendelea na masomo kwa kipindi hicho kutokana na Mpanje kushindwa kuwalipiwa ada kwa vile korosho haikutoa mavuno mazuri.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa