Home » » ASILIMIA 28 YA WAKAZI DOM HAWANA VYOO

ASILIMIA 28 YA WAKAZI DOM HAWANA VYOO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
ASILIMIA 72 ya wananchi wa mkoani Dodoma hawana vyoo bora huku asilimia 28 wakijisaidia katika vichaka na maeneo ya wazi.
Haki hiyo inaelezwa kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira na kuhatarisha usalama wa afya za wananchi katika wilaya zote mkoani hapa.
Ofisa Afya Mkoa wa Dodoma, Edward Ganja, alibainisha hayo juzi mjini hapa katika mafunzo kwa waandishi wa habari yaliondaliwa na Shirika la Plan Internatinal.
Alisema utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mapema mwaka huu mkoani Dodoma unaonyesha idadi kubwa ya wananchi hususan vijijini wamejenga vyoo visivyo na ubora ambavyo ni hatari kwa usalama wa afya.
“Ukiona mabanda ya vyoo ni yale yaliyojengwa kwa makuti bila kupauliwa ambayo hujulikana kama ‘pasipotisaizi’ ambapo hakuna faragha kwa kuwa mtu akiingia sehemu ya kichwa huonekana wazi,” alisema Ganja.
Alieleza kuwa wilaya za Kongwa, Chamwino na Bahi zinaongoza kwa vifo vingi vya watoto walio chini ya miaka mitano kutokana na kukosa vyoo bora na kusababisha vinyesi kutapakaa sehemu za wazi, mashambani, kwenye vyanzo vya maji na kwenye makazi ya watu na kusababisha milipuko ya magonjwa.
“Kweli juhudi kubwa zinahitajika kuwahimiza wananchi kwani utafiti unabainisha asilimia 27 tu za kaya zenye vyoo bora katika mkoa wa Dodoma, hii ni hatari sana,” alisema Ganja.
Aidha, aliwataka wananchi kutunza mazingira kwa kujenga vyoo bora na kuachana na tabia ya kujisaidia sehemu za wazi.
Kwa mujibu wa Shirika la Plan Internatinal Watanzania watoto 36,500 wakiwemo watoto 18,500 wanapoteza maisha kutokana na kuharisha na asilimia 90 kuugua kutokana na maji machafu, mazingira machafu na kushindwa kunawa vizuri kabla na baada ya kutoka chooni.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa