VIONGOZI
wa halmashauri nchini kwa kushirikiana na waganga wakuu wametakiwa
kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyotolewa na serikali kupitia Bohari
Kuu ya Dawa (MSD) vinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.
Agizo hilo lilitolewa mjini hapa jana na Naibu Waziri Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, katika ziara ya kwanza
tangu ateuliwe kuwa waziri akiongozana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma za Jamii katika kukagua taratibu za usambazaji wa dawa, vituo na
hospitali za serikali Masasi, mkoani Mtwara.
Kebwe alisema kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu huhusu utumiaji
mbaya wa dawa hizo, jambo linalowakosesha huduma bora wananchi na kukosa
imani na serikali yao.
Alieleza hali hiyo inatokana na baadhi ya watendaji na wafanyakazi
kutokuwa waaminifu na kutimiza wajibu wao, hivyo kuchangia kwa kiasi
kikubwa kuwapaka matope hata wasio na tabia hiyo.
Alitumia fursa hiyo kuzitaka hospitali za serikali kutumia vyanzo
vingine vya mapato ili kununua dawa na vifaa tiba katika kuongezea
matumizi mbalimbali na bajeti ya serikali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margaret
Sitta, alisema ni muhimu suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
kupewa kipaumbele cha hali ya juu kutokana na kuwa ndio msingi wa huduma
bora za afya kwa jamii.
Sitta alisema kutokana na ufanisi mkubwa uliopo katika upatikanaji wa
dawa hospitalini na vituo vya afya baada ya mfumo wa ufikishaji dawa
moja kwa moja hadi vituoni (DD) unaofanywa na MSD ni vizuri serikali
kutambua kuwa ufanikishaji wa hatua hiyo unahitaji uwezeshi hasa wa
fedha, hasa bajeti kufika kwa wakati.
Mjumbe wa Bodi ya wadhamini MSD, Dk. Ahmed Hingola, alisema endapo
serikali itadhibiti na kuhakiki dawa chache zilizopo, ili kutekeleza
mahitaji ni wazi lawama za wananchi kwa bohari ya dawa zitakwisha.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment