Kila kukicha miongoni mwa kero kubwa ambayo imekuwa ikiumiza vichwa kwa Watanzania imekuwa ni umeme.
Mbaya zaidi licha ya hivi karibuni kupandishwa gharama za huduma hiyo, bado nishati hiyo imeshindwa kuboreshwa.
Aidha, kasi ya uwekezaji katika sekta ya nishati
nchini imeendelea kukua huku makadirio ya mtaji katika uwekezaji
ikikadiriwa kufikia zaidi ya dola za Marekani 4 bilioni hivi karibuni.
Kiasi hiki cha fedha kiliingizwa kupitia mzunguko wa shughuli mbalimbali
za utafutaji, uchimbaji na uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia gesi
asilia.
Baadhi ya miradi katika mzunguko huo ni pamoja na
ule wa bomba la gesi uliotumia zaidi ya dola 1.2 bilioni. Mradi huo
unatarajiwa kuleta mapinduzi katika nishati ya umeme nchini, ikitegemewa
kuwa utaongeza megawati 3,570. Utaanza kwa kuzalisha 900 ifikapo 2015.
Wakati harakati hizo zikiendelea, hivi karibuni
Tanzania iliwakutanisha zaidi ya wadau 200 kutoka kampuni mbalimbali za
nishati ya umeme wa ndani na nje ya nchi kupitia mkutano wa ‘Powering
Africa Tanzania’, ulioandaliwa na taasisi ya EnergyNet inayojihusisha na
mikakati ya utekelezaji na uwezeshaji wa sekta ya nishati ya umeme
barani Afrika.
Mkutano huo ulilenga kuangalia mazingira ya
uwekezaji na uboreshaji wa huduma za nishati ya umeme ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Marekani Barack Obama kwa nchi sita za
Afrika.
Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wadau
katika mkutano huo, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
anasema muda wa Watanzania kuteseka na changamoto ya ukosefu wa nishati
ya umeme utamalizika muda mfupi ujao kutokana na hatua mbalimbali
zilizofikiwa mpaka sasa katika upatikanaji umeme.
“Tunaelekea kuandika historia katika la Afrika
kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo tatizo la uhaba wa umeme
halitakuwepo; kwa sasa kuna miradi mbalimbali inayoendelea ambayo mingi
itakamilika mwishoni mwa mwaka huu. Kati ya miradi hiyo ni bomba la gesi
kutoka Mtwara, lakini pia kuna mabadiliko ya kulifumua na kuliunda upya
shirika letu la Tanesco, tayari tumefikia hatua muhimu,” anasema
Profesa Muhongo.
Kufumuliwa kwa Tanesco
Akizungumzia mchakato wa kufanya mabadiliko katika
shirika hilo, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
anasema mpaka sasa mchakato huo umefikia hatua nzuri.
“Mchakato wake utatoa dira kamili mwezi Juni mwaka huu baada ya kukamilika kwa hatua zinazoendelea mpaka sasa,” anasema.
Anaongeza kuwa mpaka sasa Tanesco ina jumla ya
vifaa na mitambo yenye thamani ya Sh4 trilioni hivyo inawalazimu kuwa
makini katika mabadiliko hayo.
“Madeni ya Tanesco tutayachukua Serikali kwa asilimia mia moja
lakini kuna suala la utendaji wa Tanesco kuzalisha na kuuza umeme, hiyo
haiwezekani majukumu yote tukawaachia; ni lazima tujue Kampuni gani
itastahili kupewa dhamana ya usambazaji,” anasema na kuongeza;
Mpaka sasa kuna hatua kadhaa zimeshaanza kufanyika
katika utekelezaji wa mchakato huo ikiwemo kuanzisha Kampuni ya
uzalishaji wa nguzo za kisasa zinazotumia zege, badala ya mbao kama
zinazotumika sasa ili kuepusha ukataji miti.
Kumalizika mikataba ya Tanesco
Tanesco imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na
Kampuni mbalimbali zilizoingia mikataba kwa ajili ya kuzalisha na
kuliuzia shirika hilo ili kuongeza tija katika huduma za nishati
nchini.Baadhi ya Kampuni hizo ni Songas Limited, Aggreko, Symbion na
IPTL.
Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa, zaidi ya
dola 27 bilioni zimekuwa zikitumika kila mwezi kulipa kampuni hizo kama
malipo ya gharama za umeme unaoingia kwenye mgawanyo.
Mikataba hiyo imekuwa ni sehemu ya mwiba
unaolididimiza shirika hilo la Tanesco; shirika hilo linanunua umeme huo
ikiwa ni wastani wa senti 42 kwa unit moja huku Tanesco ikiuza kwa
hasara ya senti 12 za Marekani kwa wateja wake.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba anasema
baadhi ya kampuni hizo zinatarajiwa kumaliza mikataba yake mwishoni mwa
mwaka huu, hali ambayo itachangia kupunguza mzigo katika shirika hilo.
“Mpaka kufikia mwezi Oktoba kampuni zilizoko kwenye mikataba hiyo itakuwa imemaliza mikataba yao,” anasema na kuongeza;
Lakini Kampuni ya IPTL tayari imeshaanza
kubadilisha mitambo yake ya kuzalishia umeme kwa njia ya mafuta kwenda
uzalishaji wa njia ya nishati ya gesi asilia, na mpaka kufikia mwezi Mei
mwaka huu watakuwa wamefikia kiwango cha asilimia 50 katika
ubadilishaji wa mitambo hiyo,” anasema.
Anasema kukamilika kwa hatua hizo, kutaendana na
hatua nyingine ya kukamilika kwa miradi mbalimbali, hivyo tumaini la
kuingia kwenye mapinduzi ya nishati litakuwa limeanza kutimia.
Nini kifanyike kwa sasa
Dk Prosper Ngowi kutoka Kitengo cha Uchumi, Chuo
Kikuu cha Mzumbe anasema kutokana na changamoto ndani ya shirika hilo,
ni muhimu likabinafsishwa na kuwa chombo huru bila kuingiliwa na mikono
ya kisiasa.
Akashauri pia kwamba kwa sasa Tanesco inatakiwa kuanza maandalizi ya kujiimarisha, kabla ya kubinafsishwa; hiyo itasaidia kuharakisha maendeleo, kuliko ilivyo sasa.
Chanzo;MwananchiAkashauri pia kwamba kwa sasa Tanesco inatakiwa kuanza maandalizi ya kujiimarisha, kabla ya kubinafsishwa; hiyo itasaidia kuharakisha maendeleo, kuliko ilivyo sasa.
0 comments:
Post a Comment