Home » » Waziri ashauri halmashauri,waganga matumizi dawa za MSD

Waziri ashauri halmashauri,waganga matumizi dawa za MSD

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe Stephen Kebwe
 
Serikali  imezitaka halmashauri nchini kushirikiana na waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyotolewa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) vinatumika ipasavyo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe Stephen Kebwe  wilayani Masasi, mkoani Mtwara.

Aliyasema hayo  wakati akiwa na Kamati ya Bunge Huduma za Jamii kukagua taratibu za usambazaji dawa vituo vya afya  na hospitali za serikali.

Alizitaka  hospitali za serikali kutumia vyanzo vingine vya mapato ili kumudu kununua dawa na vifaa tiba.

“Ni muhimu kuelewa kuwa hospitali ina vyanzo vingi vya mapato, wakati umefika sasa kutumia fursa hizo katika kuhakikisha mapato yanayotokana na vyanzo vya hospitali yanatumika pia katika kuongeza uwezo wa ununuaji dawa na vifaa tiba,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma za Jamii, Magreth Sitta, alisema ni muhimu suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupewa kipaumbele cha hali ya juu kwa kuwa ndiyo msingi wa huduma bora za afya kwa jamii.

Mjumbe wa Bodi ya wadhamini MSD, Dk. Ahmed Hingola, alisema ikiwa serikali itadhibiti na kuhakiki dawa chache zilizopo ili kutekeleza mahitaji, lawama za wananchi kwa MSD.

“MSD kazi yake kubwa ni upelekaji wa dawa huku usimamizi wa matumizi katika kutumika kama ilivyokusudiwa ikiwa bado ni changamoto hasa katika sehemu husika hivyo imeanza harakati za uwekaji wa nembo dawa za Serikali  ili kudhibiti dawa hizo zisiweze kupita njia za panya,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa