Home » » Waziri Pinda avunja ukimya

Waziri Pinda avunja ukimya

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amevunja ukimya na kueleza jinsi mfumo wa vyama vingi nchini umesaidia kwa kiasi kikubwa kutikisa waliopo madarakani, hadi imefikia hatua ya kupongezwa na mataifa makubwa.

Waziri Pinda alitoa kauli hiyo katika mkutano wake na viongozi wa dini, vyama vya siasa, wadau mbalimbali wa maendeleo na wawakilishi wa wananchi mkoani Mtwara jana wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu .
“Mkipata fursa ya kwenda nchi za njena wale mnaokwenda mara kwa mara wasikilizeni wanasema nini juu ya nchi yetu ni kusifu amani, ukarimu utulivu na upendo na hali hiyo inatokana na kukataa kwetu ubaguzi wa rangi, dini na ukabila ,” alisema na kuongeza;
“Hali hiyo imechangia Serikali iliyopo madarakani kukubaliana na mfumo wa vyama vingi ambavyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kutikisa waliopo madarakani na hata mataifa makubwa yanapongeza hatua iliyopo ya demokrasia ya kisiasa na uvumilivu wa serikali.”
Alisema Watanzania wenyewe hawaoni hayo kwa kuwa wapo ndani.
“Tunaambiwa eti hakuna uhuru wa habari nchini, lakini tazameni idadi ya vyombo vya habari na utitiri uliopo ambapo kila mmoja anabwaga manyanga atakavyo, leo huyu kamtukana huyu... enzi za Kambarage hakika wangeishia Tunduru, sisi ni taifa moja tushikane mkono kwenda mbele,” alisema.
Waziri Pinda, aliwataka wananchi wa Mtwara, Lindi na Tanzania kwa ujumla kutokukubali fursa ya gesi asilia ikawa kichocheo cha vurugu badala ya kuleta neema na maendeleo kwa ujumla.
Alisema kutokana na minong’ono mingi juu ya uwekezaji wa mradi huo ni muhimu kuelewa macho ya kila mmoja yapo katika nishati hiyo baada ya kubainika kuwa ndio uchumi mkuu siku zijazo kwa taifa.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi, hivyo kufikia kuwa miongoni mwa nchi 20 zenye viashiria vya kukuza uchumi ikiwa ni juhudi za Serikali kufikia hatua hiyo.
“Ujio wa wakuu wa nchi ya China na Marekani na kuahidi kuwekeza katika sekta muhimu za maendeleo umeleta maneno sana, ipo minong’ono, wengine wakihoji kwa nini Rais wa Marekani hakwenda kwao ambako ndiko asili yake,” alisema na kuongeza;
“Ukweli ni kwamba wakuu hao wa nchi wameona kuwa Tanzania ni nchi pekee miongoni mwa nchi barani Afrika iliyoonyesha dhamira ya kweli kuwaletea wananchi wake maendeleo,” alisema.
Aliwaondoa hofu wanaojiuliza kwa nini China imekuwa ikipewa miradi mingi ya maendeleo nchini, akisema ni kutokana na watu wa Taifa hilo kuwa na masharti nafuu.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa