JESHI la Polisi mkoani Mtwara limewataka wananchi kuendeleza
ushirikiano na mshikamano ili kudumisha amani na utulivu mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alitoa kauli hiyo alipozungumnza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema wakati umefika kwa wananchi wa Mtwara kusahau mambo
yaliyotokea mwaka jana na kuathiri amani na utulivu na sasa kuwaomba
wayaangalie upya na kuyatafakari kwa umakini na kuyatafutia ufumbuzi
badala ya kuyaendeleza.
Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi lipo tayari kushirikiana na
wananchi ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatumika kuwa
fursa ya kutatua kero zilizopo likiwemo lile la kukabiliana na vitendo
vya uhalifu.
Pia aliwashauri wananchi wanapokosana ni vema watumie viongozi wa
serikali za mitaa, wa dini, wa mila ama wazee maarufu katika kutatua
mashauri yanayosababisha kujigawa na yanaposhindikana wasisahau kuwa
kuna mabaraza ya usuluhishi katika kata.
Pamoja na mambo mengine, kamanda huyo alisema mwaka jana yaliripotiwa matukio 10,233 ikilinganishwa na mwaka juzi 11,910.
Alisema makosa dhidi ya binadamu mwaka jana yalikuwa 212 na mwaka
2012 yalikuwa 209 ambayo ni sawa na ongezeko la makosa matatu.
Kwa upande wa makosa dhidi ya jamii, mwaka jana yalikuwa 448 na mwaka
2012 yalikuwa 451 ambayo ni sawa na upungufu wa makosa matatu, na
makosa dhidi ya mali kwa mwaka jana yalikuwa 980 na mwaka 2012 yalikuwa
937, sawa na ongezeko la makosa 43.
Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani kwa mwaka jana kulikuwa na ajali 177 kati ya hizo ajali 89 zilisababisha vifo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment