KAYA 12 za wakazi wa Magomeni A katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani
mkoani hapa, wamekosa mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa
na mvua iliyonyesha hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara, Wilman Ndile, alisema kuwa kaya 12 hazina makazi huku
zikihifadhiwa katika Shule ya Msingi Mangoela.
Ndile alisema kuwa mvua hizo zilinyesha siku ya mkesha wa Krismasi
kuanzia saa 4 usiku hadi asubuhi na kusababisha uharibifu wa nyumba
zaidi ya 10 na kuharibu vitu mbalimbali vilivyokuwepo ndani ya nyumba
hizo vikiwemo vyakula.
Alisema kuwa walioathirika wengi ni wale wanaoishi mabondeni huku nyumba zao zikiwa sio imara.
Mkuu huyo aliwalalamikia watumishi wa Idara ya Mipango Miji Manispaa
ya Mtwara-Mikindani, ambao wamehusika na utoaji wa vibali vya ujenzi
katika maeneo ya miundombinu ya kupitishia maji ya mvua ambayo
hayakustahili kujengwa makazi ya watu.
Alisema kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa tani 250 za
mahindi huku wananchi wakilazimika kulipa sh 50 kwa kilo moja na kwa
wasio na uwezo wakipewa bure.
Mmoja wa waathirika hao, Asha Chimpume, ameiomba serikali pamoja na
wasamaria wema ambao wameguswa na tukio hili kujitokeza kuwasaidia
chakula kwa sababu kwa sasa hawana chakula kutokana na kusombwa na maji.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment