Masasi. Mkuu wa Wilaya ya Masasi, mkoani
Mtwara, Farida Mgomi amewashukia maofisa ushirika wilayani hapa kwamba
ni chanzo cha kufanya halmashauri kushindwa kukusanya mapato ya ushuru
wa mazao.
Akizungumza na madiwani na watendaji kwenye Baraza
la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi juzi, Mgomi alisema
maofisa hao wamekuwa kikwazo.
Mgomi alisema kushindwa kukusanya mapato ya ushuru
wa mazao hasa zao la korosho kwenye halmashauri zilizopo wilaya hapa,
kunachangiwa na uzembe unaofanywa na maofisa ushirika.
Alisema wameshindwa kusimamia vizuri kutoka vyama
vya msingi na kwamba, hali hiyo imekuwa ikizisababishia halmashauri
kukosa mapato.
Mgomi alisema baadhi ya maofisa ushirika wamekuwa
wakishirikiana na viongozi wa vyama vya msingi kukwepa ushuru wa
halmashauri, kitendo ambacho alidai hatakifumbia macho.
Aliongeza kuwa vyama vya msingi wilayani hapa
vimekuwa na tatizo kubwa kulipa ushuru wa ununuzi wa korosho kwa
halmashauri, vimesababisha halmashauri kupata hasara ambayo inazifanya
zishindwe kutekeleza baadhi ya shughuli za maendeleo.
“Uzembe unaofanywa na maofisa ushirika kwa
kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji ushuru wa ununuzi wa mazao hasa
korosho kutoka vyama vya msingi, kunazisababishia halmashauri zishindwe
kukusanya mapato kikamilifu,” alisema.
Alisema akiwa mkuu wa wilaya atahakikisha
anawabana maofisa ushirika wasimamie ipasavyo ukusanyaji ushuru na
kwamba, ofisa ushirika yeyote atakayebainika kufanya uzembe katika
ukusanyaji mapato, ofisi yake itahakikisha inamshughulikia.
Alisema lengo ni kuziwezesha halmashauri kuweza kukusanya mapato kama zinavyotarajia.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment