KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kimewashauri wawekezaji wa
ndani na nje kutumia fursa kinazozitoa kwa wawekezaji kuwekeza katika
sekta ndogo ya zao la korosho ili kuongeza uzalishaji wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Juliet Kairuki, alisema hayo
jana wakati wa mkutano wa wadau wa sekta hiyo na kuongeza kuwa
wanahitajika kukitumia kituo hicho ili kupata fursa zitakazowawezesha
kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa zao hilo.
“Kituo chetu kinahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kuwekeza katika sekta hii ambayo ni muhimu katika uchumi wa nchi na
ustawi wa jamii,” alisema Kairuki.
Alisema TIC imeweka vivutio mbalimbali kwa wawekezaji ambao
wamejizatiti kuwekeza katika kilimo, ikiwamo misamaha ya kodi kwa
bidhaa za mitaji.
Aliongeza kuwa Tanzania bado inahitaji wawekezaji kuwekeza katika
kilimo cha zao hilo, viwanda vya kusindika na kuyatumia masoko ya ndani
na nje ya nchi.
Sambamba na hilo, alisema Tanzania ina mfumo mzuri wa sheria ambao
unavutia kila anayetaka kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo ya
kilimo.
Mchumi Mwandamizi Kitengo cha Masoko wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Aneth Mathania, aliwaeleza wawekezaji kuwa Tanzania ina
‘barcode’ yake, hivyo wakiwekeza mazao yao hayatapata shida ya soko.
“Tanzania imeweka utaratibu mzuri kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo
katika mnyororo wake wanapata faida, wakiwamo wakulima, wasindikaji na
wasafirishaji,” alisema.
Pia alisema vifungashio vya zao la korosho vinatolewa na Shirika la
Viwanda Vidogo (SIDO) hivyo fursa ya uzalishaji wa zao hilo ni kubwa.
chanzo;tanzania daima
0 comments:
Post a Comment