KAMATI Tendaji ya Taifa ya Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (Tasaf), imewahimiza viongozi kutambua umuhimu wa kuishirikisha jamii
katika kuibua na kuchangia utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yao ili kuifanya
kuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi.
Akizungumza na wanavijiji wa Imekuwa na Majengo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, Makamu mwenyekiti wa
kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema kuwa
hali hiyo itasaidia kuwafanya wananchi kuibua na kuendeleza miradi mingi ya
maendeleo na kujiondolea umasikini.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, Kandoro
alisisitiza umuhimu wa kuikamilisha kwa wakati ili kuwasaidia walengwa.
Kandoro aliongeza kuwa hivi sasa Tasaf iko katika
hatua ya utekelezaji wa miradi ya awamu ya tatu, inayolenga kuziokoa familia
masikini katika zaidi ya kaya milioni 1.2 zinazokabiliwa na umasikini ifikapo
mwaka 2015.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus
Mwamanga aliwapongeza wakazi wa vijiji vya Imakuwa na Majengo kwa jitihada zao
za kuibua mradi wa zahanati ya Imakuwa ambayo imejengwa kwa fedha toka Tasaf na
mchango wa nguvu za wananchi wa vijiji hivyo na kuwatatulia tatizo la kusafiri
umbali wa zaidi ya kilomita nane kufuata huduma za afya.
Baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo, waliipongeza
Tasaf kwa kuwezesha miradi ya maendeleo inayoibuliwa na wananchi nchini bila
ubaguzi.
Kamati Tendaji ya Taifa ya Tasaf, tayari imekagua
miradi minne katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashaura ya Mtwara
ambako Tasaf imechangia sh bilioni 6 kuendeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu
mbalimbali katika nyanja za elimu, afya, barabara, uzalishaji mali na uwekezaji
katika halmashauri hizo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment