Home » » TAASISI ZAHIMIZWA KUWATUMIA WAJASIRIAMALI WADOGO

TAASISI ZAHIMIZWA KUWATUMIA WAJASIRIAMALI WADOGO

 Taasisi za umma, makampuni binafsi yamehimi zwa kuwatumia wajasiriamali wadogo wanawake kuwapa huduma mbalimbali wanazohitaji ili kuwajengea uwezo badala ya kufuata huduma hizo katika makampuni makubwa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Entango, Bi. Emma Kawawa, ambayo pamoja na kuwekeza katika masuala ya biashara lakini pia imekuwa ikijihusisha na kuwainua wajasiriamali wadogo wanawake kwa kuwajengea uwezo katika nyanja ya elimu na mitaji, wakati akimkaribisha mgeni rasmi kufunga mafunzo ya siku tano ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na kampuni yake.
Bi. Emma alisema kuwa ni vyema makampuni yanayokuja Mtwara sasa kuwekeza katika nyanja mbalimbali wakawatumia wajasiriamali wadogo wanawake katika kutoa huduma mbalimbali kama chakula, usafi na huduma ya usaidizi katika maofisi yao kwani sasa wameshapata utaalamu wa kutosha katika maeneo hayo.
"Naomba serikali ilione hili hawa akinamama ambao leo wanahitimu mafunzo ya biashara ya wiki tano wameiva vizuri katika kutoa huduma lugha nzuri na namna ya kuyaweka maeneo yao ya biashara sasa hebu watumieni hawa badala ya kwenda kutafuta huduma kama hizo mbali au katika makampuni makubwa," alisema Emma.
Akihutubia hivi karibuni katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha ualimu mjini hapa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw.Pansiaono Nyami, alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo wanawake na hivyo haitawaacha nyuma bali itawashirikisha katika kila jambo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Bw.Nyami alisema kuwa serikali katika ngazi zote imekuwa ikiwashirikisha wajasiriamali kwa kuwapa taarifa mbalimbali muhimu kwao pamoja na kuwaunganisha na fursa zinapotokea ili kuwaongezea wateja na hivyo kukuza mitaji yao.
"Na leo hapa nataka nikuambieni kwamba mkuu wetu wa mkoa ambaye ndiye aliyenituma kuja hapa kwa niaba yake amesema hivi tena ameongeza haya maneno kwa kuandika kwa mkono kwenye hii hotuba yake ninayoisoma kwenu kuwa iwapo mtaonesha nia ya kuanzisha saccos yenu yenye sura ya Kimkoa nitawapa shilingi milioni tano kama kianzio, jamani hii mnaionaje," alisema Nyami.
Kampuni ya Entango ambayo imejikita katika uwekezaji katika maeneo mbalimbali hapa mkoani imekuwa ikijihusisha na kuwainua wajasiriamali wadogo baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa wajasiriamali hao hawana uwezo wa mtaji na elimu ya biashara hali inayowafanya kushindwa kushindana katika biashara na shughuli mbalimbali wanazozifanya

chanzo;majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa