Home » » Simbakalia awapa somo madiwani

Simbakalia awapa somo madiwani


MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph Simbakalia, amewataka madiwani kufuatilia mafunzo kwa umakini ili kupata fursa ya kujadili na kuelewa ni jinsi gani mpango wa kunusuru kaya maskini unatekelezwa.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja inayojumuisha mafunzo ya siku nne ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya tatu ya TASAF, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parishi.
 Alisema Madiwani ni watumishi wa wananchi ndiyo maana wanapaswa kusimamia maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
“Wote tunakumbuka kwamba mpango huu ulizinduliwa rasmi  na Rais Kikwete  Agosti 15, 2012 mjini Dodoma na wakati wa uzinduzi  huo, rais alionyesha kuridhishwa kwake na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa awamu mbili za TASAF zilizotangulia na akaagiza awamu ya tatu ya TASAF iendeleze yote yaliyopatikana pamoja na kuongeza ubunifu kwa jinsi watakavyoweza kutambua walengwa wa mpango huu,” alisema.
 Alisema walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini ni zile kaya maskini na zilizo katika mazingira hatarishi kwenye vijiji na mitaa na kaya hizo zitafaidika kwa kushiriki katika mpango wa jamii wa uhuwilishaji fedha.
Aidha alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, mpango huu unatarajia kuwafikia walengwa milioni 7.5 katika kaya milioni 1.2.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa