MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), utaanza kutoa zawadi kwa
halmashauri zitakazoandikisha kaya nyingi katika Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF).
Hayo yalibainishwa juzi na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya mfuko
huo, Charles Kajege, katika mkutano wa wadau wa NHIF na CHF uliofanyika
kwenye ukumbi wa Makonde Beach mjini hapa.
Kajege alisema Menejimenti ya NHIF inakamilisha mapendekezo hayo na
wao katika bodi wayaangalie, ili kusudi iwe ni kichocheo cha kufikia
afya bora kwa wote.
Alisema vigezo vitatangazwa na wamewaambia waangalie namna wadau
watakavyoshiriki katika jopo la majaji watakaoendesha zoezi la kuwapata
washindi kitaifa na tuzo hiyo wataiita ‘Social Health Insurance For
All Award’.
Alisema malengo ya kitaifa ya CHF ni kila mkoa na halmashauri waweke
mikakati ya kuifikia, kwani ni agizo la serikali kuwa ifikapo mwaka
2015 Watanzania wanaohudumiwa na NHIF na CHF ifikie asilimia 30.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Mtwara, Joyce Sumbwe, aliwaomba viongozi wa
serikali ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri, suala la NHIF na CHF
kwao liwe ajenda kwenye vikao vyao na wanapokutana na wananchi
wawasisitizie juu ya kujiunga na mifuko hiyo, ili wanapougua iweze
kuwasaidia.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, aliwataka
wanachama wa NHIF na CHF kutumia kadi zao za matibabu kwa kuzingatia
taratibu zilizopo, waache mtindo wa kuazimishana kadi za matibabu au
hata kufanya biashara ya kadi hizo kwani kufanya hivyo ni kinyume na
sheria za mfuko.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment