Home » » Halmashauri Masasi ielimishe wananchi umuhimu wa misitu

Halmashauri Masasi ielimishe wananchi umuhimu wa misitu


 
KWA muda mrefu sasa wadau wa misitu wamekuwa wakilalamika juu ya kuwapo hekta kadhaa za misitu inayopotea kila mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na uharibifu na kuvunwa kiholela.
Wadau hao wa misitu wamekuwa wakitoa hadhari juu ya athari zitokanazo na kupotea kwa misitu, ikiwa ni pamoja na ongezeko la joto duniani, mabadiliko ya hali ya anga kwa rekodi ya kipimo joto, kupanda kwa maeneo yenye maji baharini na kuwapo mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa ujumla athari hizo na nyingine zinasababishwa na uharibifu dhidi ya misitu huku zikihitajika jitihada za haraka za kukabiliana na hali hiyo.
Licha ya kwamba maisha ya binadamu hutegemea mazingira yanayomzunguka kujikimu hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa kupitia misitu mvua hunyesha na kusababisha ustawi na ongezeko la chakula na ndivyo asilimia kubwa ya watu hutegemea kilimo kujipatia mahitaji ya kila siku, hivyo katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wingi ni lazima misitu ilindwe kwa nguvu zote katika ukuaji na ustawi wa jamii.
Wapo wadau kama Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) ambao wamesema wastani wa hekta 40,000 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na shughuli za binadamu huku katika maeneo mengine, wakiwapo wavunaji haramu wa bidhaa hizo na kuendelea kutishia uhai wake.
Misitu ya Tanzania ina umuhimu wa asili kama nchi, kitaifa na kimataifa ambapo ni ya siku nyingi yenye aina nyingi za miti na wanyama wanaopatikana katika misitu hiyo na si mahali pengine duniani.
Wiki iliyopita nilikuwa katika ziara wilayani Masasi mkoani Mtwara kuangalia hali ya uhifadhi wa misitu na wajibu wa wananchi katika kulinda rasilimali hiyo.
Ziara hiyo ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa mama misitu ambao unalenga kukuza uwajibikaji katika utunzaji misitu nchini, chini ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).
Kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini, wilaya ya Masasi inahitaji kutoa elimu thabiti kwa wananchi juu ya usimamizi na uhifadhi wa rasilimali hiyo pamoja na kuweka bayana faida zitokanazo nayo.
Katika baadhi ya vijiji nilivyotembelea ambavyo vimepakana na misitu, wananchi walionesha waziwazi kutojua umuhimu wa kutunza rasilimali hiyo huku kukiwa hakuna hata kijiji ambacho kinamiliki msitu wake wenyewe na unaoweza kuwapatia mapato kijijini hapo.
Hali hiyo inasababisha wananchi kuona wametengwa wasiojua nini umuhimu wa rasilimali hiyo na vijiji vingine vikijua kama rasilimali hiyo ni ya halmashauri peke yake na wao hawana umuhimu katika eneo hilo.
Kwa mfano viijiji vya Sindano, Mkwapa, Namalembo na Mgangala, vyote vimepakana na misitu ya asili lakini hakuna kijiji hata kimoja kinachomiliki msitu wake chenyewe na kujua mapato yatokanayo na bidhaa hiyo, kama yanaweza kuendeleza kijijini hapo, jambo ambalo wamebakia kuona kama wako pembeni.
Ni kutokana na hali hiyo, kila wanapoingia wavamizi na kuvuna holela katika msitu huo wananchi hubakiwa kusema wanasikia hupata vibali kutoka halmashauri hivyo wao huwaacha na kuendelea na shughuli zao.
Kwa kutambua umuhimu wa rasilimali hiyo, ni vema halmashauri hiyo ikasogeza huduma ya elimu zaidi kwa wananchi wake, vilevile ikaharakisha mpango wa matumizi bora wa ardhi ambao utasaidia wananchi wa vijiji hivyo kujua mipaka ya eneo lao na matumizi yake.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa