Home » » Mradi wa gesi Mtwara wafikia pazuri

Mradi wa gesi Mtwara wafikia pazuri

WIKI iliyopita wadau wa maendeleo wakiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini walitembelea mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ilianza kwa kutembelea eneo la Kinyerezi, Ilala jijini Dar es Salaam ambako kutajengwa mitambo ya kupokea gesi itakayokuwa inasafirishwa kutoka Mnazi Bay, Mtwara na Songosongo, Kilwa tayari kuzalisha umeme.
Ujenzi huo unafanywa na Kampuni ya China Petroleum Technology Development Corporation (CPTDC), ikisaidiana na Kampuni za China Petroleum Pipeline Bureau (CPP) na China Petroleum Pipeline Engineering Corporation (CPEC).
Katika eneo hilo la Kinyerezi, ujenzi wa mtambo wa Kinyerezi I ulikuwa ukiendelea kwa kasi ya ajabu na unatarajia kukamilika mwakani Agosti tayari kwa kuanza kupokea gesi ili kuzalisha umeme wa megawati 300. Pia mtambo wa pili, Kinyerezi II unatarajiwa kuanza ujenzi wake katika siku za hivi karibuni. Baada ya mwaka mmoja na nusu utakamilika na kuzalisha umeme wa megawati 240.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi anasema Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Desemba mwakani ukihusisha ujenzi wa bomba kubwa la inchi 36 na litakuwa linasafirisha gesi yenye ujazo wa futi 784 milioni kwa siku, zenye uwezo wa kuzalisha megawati 3,570 za umeme.
Anasema bomba hilo linalojengwa kwa umbali wa kilometa 548 ambapo kati ya hizo, kilometa 487 zitakuwa ni nchi kavu na bomba jingine la kipenyo cha sentimeta 24 litajengwa kwa urefu wa kilometa 24 baharini katika eneo la Somanga Fungu ambalo litaungana na bomba kuu kutoka Mtwara.
“Kiasi hicho cha umeme kitakuwa kikubwa kuzalishwa nchini kwani kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati kati ya 900 na 1,000 wakati matumizi ni takribani megawati 840 kwa siku,” alisema. Pia kutajengwa mitambo minne ya Tanesco yenye uwezo wa kuzalisha megawati 840, Pia kutajengwa bomba la gesi litakaloenda mikoani.
Mikoa ambayo imeainishwa kwenye mradi huo ni Morogoro, Tanga, Moshi na Arusha. Katika ziara hiyo, wadau hao walitembelea maeneo mbalimbali na kuangalia hatua za ujenzi wa bomba hilo, ikiwa ni pamoja na kuunganishwa kwa mabomba tayari kwa kuchimbiwa chini.
Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Worley Parsons, Pieter Erasmus ambayo inasimamia ujenzi wa bomba hilo anauhakikishia umma wa Tanzania kuwa bomba hilo litakuwa kati ya mabomba ya gesi ya kisasa duniani. Anasema ujenzi huo unaenda kwa kasi inayotarajiwa ambapo utakamilika kwa muda uliopangwa kwa nia ya kuwezesha Watanzania kufaidika na ujenzi huo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa bomba hilo kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa upande wa Mabomba, Balthazar Thomas anasema baada ya kumaliza kuunganisha bomba, kazi itakayofuata ni kuchimba mtaro na kulitandika. Anaamini kwamba hadi Julai mwakani kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Anasema kuanzia Septemba 26 mwaka huu walianza kazi ya kuunganisha mabomba hayo na hadi kufikia wiki iliyopita tayari mabomba yenye urefu wa kilomita 142 kati ya 542 yalikuwa yameunganishwa. Kazi hiyo inafanywa na vikosi sita vilivyoko katika maeneo mbalimbali na kila kikosi kinaunganisha kilometa nne kwa siku na baadaye kukutana katikati hivyo baada ya siku 100 itakuwa kazi hiyo imekamilika.
Kati ya vikosi hivyo, kimoja kiko katika eneo la Somanga Fungu ambako bomba litapita chini ya bahari umbali wa kilomita 25 na kwamba kati ya hizo, kilometa tano ziko pembezoni mwa bahari. Anasema tayari mabomba yatakayojengwa baharini yameongezewa uzito kwa kutumia zege toka kilometa tano hadi 11.
Uzito huo unafanya mabomba yawe imara baharini kwa kukaa chini ya uso wa baharini ambapo yataingizwa baharini kwa kutumia reli maalum ambayo tayari imeshajengwa. Inaelezwa kwamba tayari kuna kikosi maalum kwa ajili ya kupindisha mabomba hayo katika maeneo ya mabonde na milimani.
Thomas anazidi kubainisha kuwa kupitisha bomba chini ya bahari hakutaathiri mazingira kwani kabla ya kuanza mradi kulifanyika tathmini ya mazingira na kupewa kibali. Katika ziara hiyo pia wadau hao walitembelea Kitongoji cha Mchepa katika Kijiji cha Madimba, wilayani Mtwara ambapo kitakuwa kitovu cha mradi wa uchimbaji wa gesi asilia.
Katika eneo hilo tayari maandalizi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi 86 umeanza zikiwemo nyumba tatu za wakuu wa kuendesha mitambo na wageni watakaotembelea eneo hilo. Msimamizi wa Ufundi wa Mitambo ya gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Sultan Pwaga anasema kuna makundi manne ya nyumba.
Anasema nyumba zimejengwa mita 40 toka eneo la kuzalisha gesi kwa nia ya kuwafanya wafanyakazi kukaa karibu na mitambo kutokana na kuwa mitambo hiyo itafanya kazi saa 24 na wafanyakazi watakuwa wakisimamia muda wote. Pwaga anasema sehemu ya kwanza ya ujenzi huo imeishakamilika kuanza kupokea wafanyakazi mwezi Februari mwakani kwa ajili ya kusimamia mitambo hiyo inayotengenezwa nje na kuja kupachikwa tu nchini.
Anasema wafanyakazi wa ujenzi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto ya kuwepo kwa nyoka wengi lakini kwa kutumia utaalamu wamemwagia madini ya salfa katika eneo lote ili kuzuia nyoka wasiingie. Anasema pia wanatarajia kutoa huduma mbalimbali kwa jamii inayowazunguka ambapo wamekamilisha ujenzi wa visima vitatu vya maji vitakavyokuwa na uwezo wa kuwahudumia wanakijiji 60,000 kila siku.
“Maji haya yamesafishwa kwa kiwango cha kusafisha maji safi ya kunywa huku tukiweka matangi na bomba kwa ajili ya wananchi,”anasema. Naye Mkurugenzi wa Masoko ya Uwekezaji wa TPDC, Mhandisi Joyce Kisamo anasema mitambo itakayowekwa katika eneo hilo la Madimba inatengenezwa nje ya nchi na itawekwa tu eneo hilo.
Anasema kinachofanyika katika eneo la mitambo kunajengwa msingi imara kwa ajili ya mitambo. Anasema katika nyumba zinazojengwa ni kwa ajili ya wafanyakazi 60 pamoja na nyumba za ziada. Anasema mradi huo wa kwanza kumilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 ni muafaka kwa miaka ijayo kwa kutumia gesi asilia.
“Napenda gesi hii inufaishe nchi nzima hivyo isisafirishwe nje kwanza ila baada ya kunufaisha Watanzania kwanza kwa maeneo makubwa kutumia gesi hiyo,“ anasema. Anasema upembuzi yakinifu umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo mshauri mwelekezi ameshauri kuhusu mipango miji kuwezesha jiji lote liweze kutumia gesi asilia pamoja na mikoa ya Mtwara na Lindi.
Anasema mkakati uliopo ni kuhakikisha gesi asilia inatumika katika miji yote yenye viwanda na pamoja na maeneo (majumbani) wanakotumia kuni nyingi kama Mororgoro. Gesi inaaminika kwamba itaokoa mazingira na uchumi kwani takriban dola bilioni moja kwa mwaka zinatumika kwa ajili ya mitambo inayotumia nishati ghali ya mafuta.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, anasema katika ziara hiyo ya wadau wa maendeleo wamo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), GITZ, Benki ya Ujerumani na wadau wengineo.
Maswi anasema kazi ya kutandaza mabomba itaanza mwezi Februari mwakani na kuwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi utakuwa umekamilika Desemba mwakani, ambapo shehena ya kwanza ya gesi itafika Dar es Salaam.
Maswi anasema lengo la ziara hiyo kwa wadau wa maendeleo ni kuwaonesha ujenzi unavyoendelea kwa kuwa wengi walikuwa wakipinga na kutoamini kama itawezekana na wengine wakidhani wajenzi wa Kichina watalipua ujenzi huo.
“Baada ya kutembelea wameshuhudia ujenzi unavyotumia utaalamu wa kisasa huku mshauri mwelekezi akieleza kuwa bomba hili ni la kisasa kuliko mabomba mengine ya gesi asilia,” anasema. Anasisitiza kuwa jambo kubwa la kujivunia ni kuwa Wachina wanajenga lakini usimamizi unafanywa na Watanzania hivyo kujihakikishia usiamamizi bada ya kuisha mkataba wa miaka miwili na wao kuondoka.
Anasema katika bomba hilo kutakuwa na sehemu 16 za kufungulia gesi hivyo Watanzania wote ni wadau kuhakikisha usalama wa gesi kwani gharama za gesi ni nusu ya dizeli.
Anasema katika sehemu hizo Watanzania watapata nafasi ya kutumia gesi. Anasema ujenzi wa bomba hilo ulianza Agosti 15 mwaka huu na ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 18 na kugharimu shilingi trilioni 1.9 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China. Naye Kamanda wa Polisi Usalama wa Madini na gesi, George Mayunga, aliyeambatana na msafara huo anawahakikishia Watanzania kuwa bomba hilo litakuwa na usalama wa kutosha.
Anasema kwa sasa katika ujenzi licha ya kuwepo na utulivu lakini katika kila kikosi wanaambatana na askari wawili wanaohakikisha kunakuwa na amani wakati wote. Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba, anasema kukamilika kwa gesi hiyo kutasaidia katika kupata umeme wa uhakika.
Anasema hatua hiyo itasaidia shirika kuacha kufikiria uzalishaji bali usambazaji kwa wananchi kwani kwa sasa sh. bilioni 900 zinapotea kila mwaka kutokana na kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta. Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Symthres Pangisa anasema tangu kuanza kwa ujenzi wa bomba hilo wananchi wa Mtwara wameongeza kipato na uchumi wao kukua.
Anasema kumekuwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo la Madimba ambapo watu wanajishughulisha kupika chakula kwa ajili ya wajenzi wa nyumba na eneo la kuweka mitambo. Pia anasema kwa mwaka mmoja pato limekuwa toka shilingi 500 hadi 770 huku viwanja vikipanda bei toka miliomi moja mwaka 2012 hadi kati ya milioni 10 na 50 huku wakitoa elimu ya ujasiriamali kwa zaidi ya watu 300 ili waweze kutumia fursa zilizopo kibiashara.
Anasema uongozi wa mkoa umeanza mpango mpya wa kuufanya mkoa uweze kujengwa katika hali nzuri huku wakitoa msisitizo kwa wananchi kuwa na muamko wa kusoma ili kuweza kufaidika na miradi hiyo hasa kuongeza vyuo vya ufundi. Baada ya ziara hiyo wadau hao wa maendeleo walisema wamefurahishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa bomba hilo.
Mtaalamu wa masuala ya Nishati toka Benki ya Dunia (WB), Nataria Kulichenko-Lotz anasema wamefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa bomba hilo lakini wanaishauri serikali kuendelea kuwajengea uwezo Watanzania ili waweze kulitunza bomba hilo. Kadhalika amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa