Masasi, Katika kuhakikisha vitendo vya
uharibifu wa rasilimali za nchi ikiwemo uwindaji haramu na ukataji miti
ovyo kwa ajili ya mbao inapungua, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili
na Utalii imeombwa kushirikisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NG’Os)
katika utelekezaji wa mikakati ya uhifadhi wa rasilimali za Taifa
ikiwemo misitu.
- Ombi hilo lilitolewa jana na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma walipokuwa katika mafunzo ya siku kumi ya kuzijengea uwezo asasi hizo juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili yaliyoratibiwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF).
Wakizungumza kwenye mafunzo hayo washiriki hao
walisema serikali lazima ichukuwe hatua ya kuanza kushirikiana na
mashirikka yasiyo ya kiserikali katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu
matumizi bora na uhifadhi wa rasilimali misitu hatua ambayo itasaidia
kudhibit upotevu wa rasilimali za Taifa.
Abdulah Mbelenje, Katibu wa Asasi ya NOSODE ya
Wilaya ya Nachingwea,Mkoa wa Lindi alisema kutokana na serikali
kutekeleza programu zake za uhifadhi wa mazingira bila ya kushirikiana
na mashirika yasiyo ya kiserikali, bado jamii imeendelea kutokuwa na
ufahamu wa kutosha juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira hali ambayo
inasababisha kuwafanya wananchi waishio pembezoni mwa misitu kuvamia
rasilimali hiyo na kuharibu ovyo.
“Asasi zetu zinafanya kazi karibu na jamii, hivyo
kama zingewezeshwa vizuri na serikali kwa kupatiwa ruzuku ili kutimiza
shughuli zake na pia kupata ushirikiano wa karibu malengo ya kudhibiti
uharibifu wa mazingira yangefanikiwa na kwamba kasi ya upotevu wa
rasilimali za taifa ingepungua,”alisema Mbelenje.
Aidha Katibu huyo alisisitiza kuwa serikali iache
kutoa vibali kiholela vya uvunaji wa misitu,badala yake ishirikiane kwa
pamoja na mashirika hayo katika kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa
misitu ili tkulinda vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, mratibu wa mradi wa
ushirikishwaji jamii katika uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu
kutoka shirika hilo la WWF kanda ya Ruvuma, Nalimi Madatta alisema lengo
la kutoa mafunzo hayo kwa asasi hizo 20 kunalenga kuzijengea uwezo juu
ya uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu ikiwa ni pamoja na
kuziunganisha ili ziweze kufanya kazi kwa pamoja.
Alisema mafunzo hayo pia yalilenga kutoa elimu ya
mbinu za uanzishaji wa miradi ya ujasiriamali ikiwemo ufugaji wa kuku wa
kisasa ili na wao wakawe mabalozi katika maeneo yao wanakokwenda kuweza
kuielimisha jamii kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali hiyo
itakuwa njia mbadala kwa wananchi kujikwamua na umasikini.
Wilaya zilizopata fursa ya kushiriki katika
mafunzo hayo ni Liwale, Nachingwea, Nanyumbu na Tunduru huku kila asasi
ikiwakilishwa na wajumbe watano kutoka kwenye maeneo ambao hao
watatakiwa kwenda kusambaza elimu waliyoipata ili jamii iweze kubadilika
na kuthamini rasilimali za taifa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment