Home » » Serikali: Marufuku ng'ombe, kilimo bonde la Mitema

Serikali: Marufuku ng'ombe, kilimo bonde la Mitema

SERIKALI imepiga mafuruku shughuli zote za jamii kufanywa ndani ya Bonde la Mto Mitema ambalo ni chanzo kikubwa cha maji kwa wakazi wa Wilaya za Newala,Tandahimba na Mtwara Vijijini. Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alipotembelea bonde hilo na kukuta shughuli nyingi za jamii zikiendelea, jambo ambalo linahatarisha kupoteza uasilia wake.
Waziri Maghembe,alionekana kukerwa zaidi baada ya kukutwa mmoja wa wafugaji akiwa ameingiza ng’ombe ndani ya chanzo hicho ambacho kilianza kufanya kazi mwaka 1984.

“Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu au mwananchi yeyote kufanya kazi za jamii ndani ya eneo hili, nawaambia mkiacha tabia hii, iendelee chanzo kitakauka na wananchi hawatatuelewa,”alisema Waziri Maghembe.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Maghembe aliagizwa kukamatwa ng’ombe 30 ambao tayari walikuwa ndani ya chanzo hicho.

Baada ya ng’ombe hao kukamtwa Waziri Maghembe aliagiza wahusika wote wapigwe faini ya Sh 200,000 kila mmoja na fedha hizo zipelekwa kwenye uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Newala.

Ng’ombe hao ni mali za wafugaji Mzee Nangumi, Athuman Fayi, Navalora na Nanjalahu.

Akizunguzmia mradi huo, Waziri Maghembe alisema umebeba dhamana kubwa ya kusaidia wananchi wa wilaya tatu hivyo haupaswi kuchezewa.

Alimtaka Diwani wa Kata ya Kitangari, Ally Said (CCM) kuitisha mikutano ya hadhara na kuwaeleza wananchi uamuzi huo.

GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa