Home » » Serikali ‘yaimegea’ kampuni Nigeria gesi ya Mtwara

Serikali ‘yaimegea’ kampuni Nigeria gesi ya Mtwara

SERIKALI imesema itaipatia sehemu ya gesi ya Mtwara Kampuni ya Nigeria ya Dangote inayojenga kiwanda cha saruji kwa ajili ya kuzalisha umeme wake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kampuni hiyo inahitaji megawati 70 za umeme kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za utengenezaji saruji mkoani humo.

Profesa Muhongo alisema umeme utakaozalishwa na kampuni ya Dangote utakuwa ni mkubwa kuliko matumizi yake hivyo kuunganishwa katika gridi ya taifa kwa ajili ya matumizi mengine ya jamii.

Leo (jana) nimekutana na viongozi wa Kampuni ya Dangote ya Nigeria ambayo imepewa jukumu la kutengeza saruji katika Kijiji cha Hiyari mkoani Mtwara.

“Tumekubali kuwapatia sehemu ya gesi kuzalisha umeme wao, pia wamesema watatoa ajira nyingi kwa vijana hasa wa Kusini.

“Wamesema kwamba uwekezaji wa viwanda vya saruji utagharimu dola za Marekani milioni 500 na watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka.

“Kama Serikali tutahakikisha tunawapa malighafi zote zinazohitajika, tumechunguza kampuni hii tumegundua ina zaidi ya viwanda vikubwa 20 barani Afrika na vinafanya kazi vizuri,” alisema.

Akizungumzia utendaji wa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) alisema bado shirika hilo linahitaji kusafishwa kutokana na kuwapo watumishi wazembe na wasio na mipango endelevu.

Profesa Muhongo alisema miongoni mwa uzembe huo ndani ya Tanesco ni baadhi ya watendaji kushindwa kuwa na mipango ya endelevu ya kuhakikisha huduma zinatolewa wakati wote.

“Haiwezekani mteja akasubiria ndani ya miaka miwili hadi mitano kuunganishiwa umeme eti kwa sababu hakuna mita na nguzo. Hivi kuna haja ya kiongozi huyo kuendelea kuitwa mtumishi wa Tanesco.

“Hivi sasa tumeagiza nguzo kutoka nchi mbili ya Afrika Kusini, Zimbambwe na hapa nchini tunashughulikia, tumeagiza nje kutokana na kampuni za Tanzania kushindwa.

“Yamekuwapo na malalamiko ya Watanzania kwamba tunaagiza nguzo nje, binafsi nasema kama kuna kampuni ya kitanzania ina nguzo imara ambazo zinatosheleza mahitaji ya nchi nzima aje wizarani tuonane,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa Dangote, Alhaji Aliko Dangote alisema lengo ni kukamilisha ujenzi wa kiwanga hicho ndani ya miezi 22 na kutengeneza saruji.


CHANZO : GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa