Home » » Wanaopisha mradi wa gesi wataka malipo yao

Wanaopisha mradi wa gesi wataka malipo yao

BAADHI ya wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha Mradi wa Gesi wa Songosongo, wanaomba  wajulishwe thamani ya nyumba na mali zao kabla ya malipo kufanyika. Kauli hiyo waliitoa Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, walipozungumza na MTANZANIA kuhusu hatima ya malipo ya nyumba na mali zao baada ya tathmini kufanyika zaidi ya miaka miwili sasa.
“Tathimini ya nyumba zetu zinazotakiwa kubomolewa ilifanyika, tumeambiwa TANESCO wamefanya uhakiki na tunaweza kulipwa lakini hatujui watatulipa nini wakati hatujui tathmini kama iko sahihi.

“Wananchi tunatakiwa kuletewa hizo tathimini tuziangalie kama zinalingana na thamani halisi ya nyumba zetu, kama hazilingani tuchukue hatua kurekebisha tatizo hilo, kama ziko sawa waendelee na utaratibu wa kutulipa,” alisema Stanslaus Matiko.

Alisema tangu watangaziwe kwamba kuna mradi wa gesi unaosimamiwa na Kampuni ya Kilwa Enegy waliacha kuendeleza makazi yao na Novemba, mwaka jana walipotakiwa kuyaendeleza walifanya hivyo lakini hawajui hatima yao ni ipi.

Aliiomba Serikali kuhakikisha wananchi wanalipwa malipo yanayostahili kuepuka kusababisha vurugu kwa kuwa hakuna aliyekuwa tayari kudhulumiwa haki yake kwa maslahi ya wenye fedha.

“Serikali inatakiwa kuwa makini, hatupingi kupisha mradi wenye maslahi ya Taifa lakini haki zetu za msingi zizingatiwe, isifikie hatua watu wakakosa makazi ya kuishi,” alisema Matiko.

Akichangia hilo, Benjamin Wasonga, alisema malalamiko yao ni kutaka kujua thamani halisi ya mali na nyumba zao kabla ya malipo.

Alisema malipo yenyewe yamechelewa kwa muda mrefu hali inayosababisha wengine kuishi katika nyumba chakavu bila sababu za msingi.

“Tunaendelea kuvumilia lakini ikifika katikati ya mwezi ujao hatujalipwa tutaandamana kudai haki zetu,” alisema Wasonga.

Malalamiko hayo ya kutaka kujua thamani ya mali zao yalitolewa pia na Saidi Ngaju, aliyeonyesha wasiwasi wake kwamba hakuna dalili ya wananchi kujulishwa watalipwa kiasi gani kwa mali zao.

Wananchi hao wa maeneo ya Majohe, Mji Mpya, Kivule, Mbande na kwingineko mradi unapopita wanaiomba Serikali kabla ya kuwalipa fidia zao, wawajulishe kila mmoja analipwa kiasi gani na wakishajiridhisha malipo yafanyike.

“Wananchi waliopitiwa na mradi wanatarajia kulipwa kati ya Julai na Agosti, mwaka huu na ifikapo Desemba mradi huo wa gesi utakuwa umeshaanza, Tanesco walishamaliza kufanya uhakiki, walituletea nyaraka tunamalizia kufanya hesabu,” alisema Hamza Juma wa Kampuni ya Kilwa Energy.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa