GESI ni utajiri, vurugu huzaa maafa. Mtwara ni ghasia, chimbuko lake ni neema ambayo Mungu ametujaalia Watanzania. Sasa basi, kama uwepo wa rasilimali hiyo imegeuka mapigano badala ya faraja kwa uchumi wa nchi, ni wazi kwamba taifa lipo katikati ya matumaini na kukata tamaa (between hope and despair).
Ni matumaini kwa sababu gesi Mtwara inaleta ukombozi wa kiuchumi kwa taifa. Picha ya kukata tamaa inasababishwa na hali halisi kuwa mapigano haya kati ya wananchi na serikali, kwa upande mwingine ni kielelezo cha raia kuchoshwa na hali ya mambo yanavyoendeshwa.
Hoja ya msingi hapa siyo gesi kutoka au kubaki Mtwara, tatizo la vurugu za wananchi ni kielelezo cha namna ambavyo watendaji serikalini wanashindwa kutoa elimu sahihi kwa raia. Tunapoliangalia suala hili kwa umakini, utaona kwamba wakazi wa mkoa huo wamenyimwa kitu muhimu sana.
Ni elimu tu! Ilifaa watendaji wa serikali wawaelimishe wananchi uhalali wa kuitoa gesi Mtwara kwenda Dar es Salaam. Hilo halikufanyika, matokeo yake wakazi wa mkoa huo wakashtuka kuwaona wawekezaji wa Kichina wakiwa kazini kujenga bomba la kusafirisha gesi. Tulitarajia nini kitokee?
Je, tulitaka wananchi wa Mtwara wakae kimya tu? Yaani wawaone Wachina wakijenga bomba, halafu wanaambiwa hilo kazi yake itakuwa kusafirisha gesi yao kwenda Dar es Salaam bila wao kuambiwa chochote, wala kuelimishwa vya kutosha namna ambavyo watakavyonufaika.
Ufafanuzi wa baadaye umekuwa dhaifu kwa sababu umewakuta wananchi wakiwa na hasira kali, kwa hiyo ni vigumu kuelewa. Utaona kwamba ndiyo maana imekuwa vigumu kuelewa, pamoja na maelezo kuwa watajengewa hospitali kubwa na ya aina yake.
Utaona kwamba makosa ya elimu kutotolewa mapema, yameibua kizaazaa cha kuigawa nchi. Sasa kuna hoja zinaibuka kuwa Shinyanga nao wanaweza kusema hawataki almasi yao ichimbwe, Geita, Kahama, Tarime na kwingineko watasimama imara kudai dhahabu yao ibaki palepale.
Si kweli kwamba watu wa Mtwara ni wachoyo, kwamba hawataki gesi yao ilineemeshe taifa zima. Siwezi kuunga mkono hilo kwa sababu ipo wazi kwamba ni haohao, kwa miaka mingi wamekuwa wakichangia pato la taifa kupitia zao lao la korosho. Hawajawahi kuonesha mkono wa birika hata kidogo.
Suala la korosho halijawahi kuwa mgogoro kwa sababu wananchi wa Mtwara wanatambua faida wanazopata kupitia zao hilo. Sasa basi, makosa ya uchoyo wa elimu kwao ambayo yamefanywa na watendaji wa serikali ndiyo kichocheo cha vurugu hizi.
Takwimu za uzalishaji wa korosho zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011, zao hilo limeliingizia taifa, fedha za kigeni jumla ya Dola za Kimarekani 4.58 bilioni ambazo kwa chenji ya Shilingi yetu ni zaidi ya trilioni 7.3.
Mapitio ya ripoti za Cashewnuts Sub-sector Study ya 2003, Hali ya Uchumi 2012 na Cashewnuts Tanzania Report 2010, yanatoa mwanga jinsi korosho inavyochangia pato la taifa. Vilevile Ripoti ya Uchumi ya Mwaka 2012, iliyofanyiwa tathimini mwezi Novemba kwa mwaka husika, korosho iliingiza jumla ya Dola za Marekani milioni 151 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 242.
Hoja hiyo, itulete kwenye ukweli kuwa Wanamtwara siyo wachoyo. Wangeelimishwa na kuubeba mradi huo wa bomba la gesi kama wa kwao, wasingefanya fujo leo. Wangeuunga mkono kwa asilimia 100 kama ambavyo hawajawahi kukataa korosho zao zisitoke Mtwara.
Hata hivyo, tujifunze kupitia maandamano na ghasia za Mtwara kuwa lazima watendaji wa serikali watambue uwepo wa wananchi siku zote. Kabla ya kufanya jambo lolote linalohusu rasilimali, ni vizuri kukawa na mazungumzo pamoja na mijadala ya wazi, yaani uelimishaji umma.
Tanzania ya sasa imekuwa kubwa katika kipengele cha upashanaji habari. Watu wanajua yanayotokea kwenye maeneo mengine ya nchi yetu na hasara ambayo kama taifa tumeipata kutokana na uingiaji wa mikataba na wawekezaji wa kigeni kuhusiana na uchimbaji wa madini.
Upo mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani 76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Yaani, nizungumze kwa msisitizo kuwa dhahabu yote iliyokuwepo pale, imetoweka na wananchi wamebaki na umaskini wao. Umakini unahitajika sana!
Mtwara waelimishwe lakini na mkataba wa kusafirisha gesi kutoka mkoani kwao kwenda Dar es Salaam, wauone. Haiwezekani ikawa ni utaratibu mzuri, kuongoza wananchi bila kujua nini kilichomo ndani ya miradi ya maendeleo ambayo serikali imesaidiana na wawekezaji.
Kampuni ya Resolute ya Australia iliwekeza Dola 370 milioni (Shilingi bilioni 592) kuanzia mwaka 1998, mkataba wao ulisainiwa Juni 25, 1997. Katika kipindi cha uhai wa mgodi, yaani miaka 14, kampuni hiyo imeuza dhahabu zenye thamani ya Dola za kimarekani 3.3 bilioni (Shilingi trilioni 5.3).
Katika mgodi huo, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Jaji Mark Bomani, serikali ilivuna mrahaba wenye thamani ya Dola milioni 11 (Shilingi bilioni 17.6) na kodi nyingine Dola milioni 16 (Shilingi bilioni 25.6). Jumla kuu ya fedha ambazo iliingiza ni Shilingi bilioni 43.2.
Kwa hesabu hiyo, ni wazi kwamba wawekezaji wa kigeni, wamevuna kiasi cha zaidi ya Shilingi trilioni 5.2. Sasa pengine Mtwara wanaona gesi yao, inaweza kuwanufaisha Wachina kuliko kulisababishia taifa uimara wa kiuchumi. Kuwaondolea dhana mbaya ni vizuri kuwaelimisha, vilevile kuoneshwa mkataba.
Inawezekana pia Wanamtwara wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%), ilikuwa inapelekwa Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Juhudi za Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu kuingilia kati ndiyo kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika.
Watu wa Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?
Kuna mambo mengi ya kuogopwa ambayo yameanza kuibuliwa. Kuna ujumbe hatari sana niliusoma kwamba Wanamtwara wakiungana na Lindi, wapo tayari kujitenga na kutengeneza Jamhuri ya Kusini. Hii ni hatari sana. Gesi yetu imekuwa janga, inatuweka katikati ya matumaini na kukata tamaa.
Tukishika matumaini, basi hatutagombana badala yake tutasahihishana na kuungana kuyajenga maendeleo ya nchi yetu. Tukikata tamaa, hatutakuwa na imani na chochote, kwa hiyo suluhisho pekee kwetu litakuwa kupigana. Tukifika hapo, Tanzania haitakuwa kisiwa cha amani tena.
Ushauri mzuri ni kutoa elimu kwa wananchi, vilevile mkataba wenyewe upitiwe kisha uoneshwe kwa wananchi jinsi ambavyo thamani yake inalingana na kile ambacho kama taifa tutavuna. Vilevile ichambuliwe kama kuna ufisadi, maana kimahesabu, wastani wa kujenga bomba la gesi duniani kote kwa maili moja ni Dola milioni 1.2 (Shilingi trilioni 1.9).
Hata hivyo, mkataba wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ni Dola 2.2 kwa kilometa (Shilingi trilioni 3.5), wakati huohuo maili ni kubwa kuliko kilometa, kwani maili 1 ni sawa na kilometa 1.6. Kwa nini sisi tunalipa bei kubwa kuliko wastani wa ujenzi wa bomba la gesi duniani? Ni swali la kujiuliza.
Rais wa Uganda, Yower Museveni, aliwahi kuwaambia Waganda kuwa ugunduzi wa mafuta nchini kwao, unafaa kuwaunganisha zaidi kuliko kuwagawa. Nasi tushike kauli hiyo, gesi isitugawe, serikali ifanye juu chini kuliweka sawa suala hili.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Chanzo Global Publishers
0 comments:
Post a Comment