WAKAZI wa Mtwara wameaswa kuzungumza lugha moja ya amani, utulivu na kujipanga vizuri ili nchi isije ikakosa fursa ya matunda yatokanayo na gesi asilia.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesisitiza, kwamba yatakuwepo mabadiliko makubwa si tu katika Mkoa wa Mtwara, bali mikoa mingine ya Nyanda za Kusini kutok
ana na barabara, viwanda na huduma nyingine zitakazotokana na uwepo wa malighafi hiyo.
Pinda ambaye amesema hakuna sababu ya kukamatana mashati, alisema hayo jana wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha saruji cha Dangote, mkoani humo.
Akielezea kampuni zilizojitokeza kuwekeza, Pinda alisema kutakuwa na mitambo ya televisheni na redio ambayo kampuni tatu zimejitokeza kutekeleza hilo.
Kampuni saba zimeamua kuwekeza katika usindikaji wa korosho, nyingine zitawekeza katika maji ya kunywa. Kutakuwa na kiwanda cha mbolea kinachowekeza katika bidhaa zinazotokana na mabaki ya gesi.
Kampuni nyingine itawekeza katika kiwanda cha kutengeneza mikate. Aidha, kampuni mbili zitawekeza kwenye matangi ya kuhifadhi mafuta na moja imeamua kujenga kiwanda cha ujenzi wa boti za uvuvi huku nyingine ikiwekeza kwenye shughuli za mbao.
Bandari ya Mtwara inawezeshwa kuhudumia meli nne kubwa kwa wakati mmoja.
“Natamani na bandari ya Mikindani tuone namna ya kuiendeleza ibaki kwa ajili ya abiria badala ya kubanana kwenye bandari kubwa,” alisema Pinda.
Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali inazungumza na Serikali ya Denmark na Korea Kusini kwa ajili ya kupata meli kubwa ya abiria na mizigo itakayotoa huduma kati ya Mtwara na Dar es Salaam.
Vile vile itajengwa reli itakayosafirisha mizigo itakayoshushwa Mtwara kwa ajili ya mikoa ya Nyanda za Kusini.
Barabara.
Serikali imeendelea kuhakikishia wananchi kwamba barabara mbalimbali ikiwamo ya Mtwara- Tunduru hadi Mbinga, wamewekwa makandarasi na ifikapo mwaka 2017 iwe imekamilika.
Barabara ya Mangaka-Tunduru tayari zabuni zimeitishwa na wanahitajika makandarasi wawili. Aidha, anatafutwa Mhandisi Mshauri kwa ajili ya barabara ya Mtwara- Newala-Masasi itakayojengwa kwa kiwango cha lami.
Wakati wawekezaji zaidi ya 45 wameomba kuwekeza Mtwara kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), Waziri Mkuu alisema viwanda ambavyo viko tayari kwa kujengwa mara moja ni cha mbolea aina ya Urea na cha dawa; ambavyo vyote vitatumia malighafi ya gesi asilia ya Mtwara.
“Ili yote yawezekane, kinachohitajika ni amani. Bila amani haya yote hayatawezekana,” alisema Pinda. Kiwanda kilichowekewa jiwe, kitakapokamilika, kitazalisha mifuko 150,000 ya saruji kwa siku sawa na tani milioni tatu kwa mwaka na kuajiri wafanyakazi 1,000.
Akizungumzia vurugu zilizotokana na upinzani dhidi ya kusafirisha gesi kwa bomba kutoka Mtwara, Pinda alisema, “Hili kweli lilikuwa ni jambo kubwa mpaka la kufika kukamatana mashati? Tangu tupate uhuru tunachangiana”.
Chanzo Habari Leo
0 comments:
Post a Comment