Home » » DHAHABU YAFOKA NANYUMBU

DHAHABU YAFOKA NANYUMBU



na Hellen Ngoromera, Mtwara
MFUMKO mkubwa wa dhahabu umegundulika kuwepo katika kijiji cha Lukwika, wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara.
Hatua hiyo ilitangazwa mwishoni mwa wiki mjini hapa na Kaimu Kamishna wa Madini Kanda ya Kusini, Aloyce Tesha, alipozungumza na waandishi wa habari walioko kwenye ziara kutembelea miradi ya Wizara ya Nishati na Madini mkoani hapa.
Alisema dhahabu hiyo iligundulika wiki mbili zilizopita na tayari ofisi yake kwa kushirikiana na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) imetuma timu ya wataalamu katika eneo hilo, ili kudhibiti madini hayo ili serikali iweze kupata kodi na ushuru unaostahili kutoka kwa wachimbaji.
“Tayari wachimbaji pamoja na watoa huduma zaidi ya 7,000 wako katika eneo hilo na kwamba tushatuma wataalamu,” alisema Tesha.
Pamoja na mambo mengine, alisema mkoa wa Mtwara una aina mbalimbali za madini yakiwemo ya chumvi ambayo huzalishwa kandokando ya bahari na jasi kwenye viwanda na mengineyo.
Alisema kwa sasa kuna maandalizi makubwa ya uzalishaji wa saruji mkoani hapa.
Tesha alisema tayari kampuni ya kufanya shughuli hiyo imeshapatikana na hivi sasa iko kwenye hatua za mwisho kuanza kazi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Fadhil Kilewo, alisema lengo la ziara hiyo ni kuwawezesha waandishi wa habari kujifunza masuala mbalimbali ya wizara hiyo na kuihabarisha jamii kwa ufasaha.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa