Home » » KUSINI SASA KUPATA UMEME KWA BEI CHEE

KUSINI SASA KUPATA UMEME KWA BEI CHEE

Na Gabriel Mushi, Mtwara
WIZARA ya Nishati na Madini, imetoa kibali kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kanda ya Mtwara, kwa ajili ya kuidhinisha kuanza utekelezaji wa ahadi ya kupunguza gharama za kufunga umeme kwa wakazi wa mikoa ya Kusini.

Kauli hiyo ilitolewa mkoani hapa jana na Meneja Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Umeme, kwa kutumia gesi, Mkurunguma Chinumba, wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea mitambo ya uzalishaji umeme ya kituo hicho.

Chinumba aliwataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, kuchangamkia fursa hiyo, kwa kuwa mpango huo ni wa muda mfupi.

“Jana (juzi) tulipokea waraka maalumu, unaotutaka kuanza kutekeleza ahadi hiyo kwa wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi.

“Kwa maana hiyo kuanzia sasa wakazi hawa, watapatiwa umeme kwa gharama za bei nafuu kama ilivyotangazwa hapo awali,” alisema.

Kwa mujibu wa Chinumba chini ya mpango huo, wananchi watafungiwa na kupatiwa huduma zote za umeme kwa gharama ya Sh 99, 000 tu.

“Punguzo hili litadumu kuanzia sasa hadi Disemba mwaka huu, ndio maana tunatoa wito kwa wakazi wetu kuchangamkia fursa hii ya kipekee.

“Hii ni fursa maalumu kwa wakazi wa mkoa huu, kwa sababu kama mnavyofahamu, umeme unaozalishwa katika kituo hiki cha Mtwara unatokana na gesi.

“Lakini pia kituo hiki sasa kinauwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 18, wakati mikoa ya Lindi na Mtwara, inatumia umeme wa Megawati 12.5.

Alisema kituo hicho kipo katika mikakati kabambe ya kupanua wigo wa uzalishaji, pamoja na miundombinu yake, kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa viwanda mbalimbali.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa