Na. Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara
Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, ameipongeza Wizara ya Fedha
kufuatia mpango wake unaolenga kuwapa wananchi uelewa wa masuala ya
Fedha ikiwemo Usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji akiba uwekezaji, kinga
za kibima na Mikopo iliyo salama kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.
Mkuu
huyo wa Mkoa ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wataalamu wa
masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi shiriki,
waliomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kutambulisha mafunzo hayo
yatakayoendeshwa katika Wilaya zote za mkoa wa Mtwara.
"Naipongeza
sana Wizara ya Fedha ikishirikiana na Taasisi nyingine zikiwemo Mamlaka
ya Usimamizi wa Bima, Benki Kuu, Masoko ya Mitaji na Dhamana na Ofisi
ya Rais-TAMISEMI, kwa kufika katika mkoa wetu kutoa elimu ya matumizi
sahihi ya fedha itakayowasaidia wananchi kutumia fedha kwa ajili ya
shughuli za maendeleo" Alisema Kanali Sawala.
"Nimeambiwa
pia kuwa wananchi watapata elimu inayohusu masuala ya mikopo, nitumie
pia nafasi hii kuendelea kuwashauri wananchi wanaohitaji mikopo kwenda
kukopa kwenye Taasisi rasmi zilizosajiliwa kisheria kwa ajili ya usalama
wa fedha zao” alisisitiza Kanali Sawala
Aidha,
aliwaasa watoa Huduma Ndogo za Fedha Mkoani Mtwara na kwingineko
kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za
Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019, na kuonya kuwa
watakaotoa huduma hizo bila kufuata sheria watawajibishwa kwa mujibu wa
sheria tajwa.
Kwa
upande wake Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya
Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alieleza kuwa lengo la
mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi, kutokana na wengi wao kuwa
na matumizi yasiyo sahihi pale wanapopata fedha.
"Programu
hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali,
ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya kupata huduma za
fedha namna ya kuzisimamia fedha zao pamoja na kujiwekea utaratibu wa
kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya kupata faida endelevu. amesema
Kimaro.
0 comments:
Post a Comment