Wakala wawili wa Tigo Pesa wajinyakulia TZS 15 milioni na TZS 10 milioni kila mmoja.
Tigo pia yatoa mamilioni ya fedha kama bonasi na zawadi kwa mawakala 2,281.
Kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali Tanzania, Tigo leo imegeuza mawakala wawili wa Tigo Pesa kuwa mamilionea katika promosheni yake iliyofika tamati leo.
Roida Kipinya, Wakala wa Tigo Pesa kutoka wilaya ya Newala, mkoani Mtwara aliyepokea kitita cha TZS 15 milioni kutoka Tigo amesema, ‘Nimejawa furaha kubwa kwa kupokea zawadi hii kubwa kutoka Tigo Pesa kama shukrani kwa juhudi zangu za uwakala. Sasa nitaweza kukamilisha mahitaji yangu muhimu ya nyumbani pamoja na kupanua biashara zangu.’
Kwa upande wake, Mojelwa Mlinga wa Pugu Mnadani jijini Dar es Salaam ambaye ameshinda TZS 10 milioni katika promosheni hiyo iliyodumu kwa kipindi cha mwezi mmoja, aliielezea promosheni hiyo kama ya kwanza na ya kipekee kuwahi kutolewa na mtandao wowote ule wa simu kwa mawakala wake nchini.
Akiongea na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi iliyofanyika katika ofisi za makao makuu ya Tigo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Bw Simon Karikari alisema kuwa nia kuu ya promosheni hiyo ilikuwa ni kurudisha shukrani kwa mawakala wa Tigo Pesa katika kipindi cha sikukuu na Mwaka Mpya. ‘Nina imani kuwa tumefanikisha malengo na ndoto za mawakala wetu katika kipindi,’ alisema.
Naye Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed alisema kuwa Tigo imetoa zawadi na bonasi kwa mawakala 2,281 kutoka sehemu mbali mbali za nchi. ‘Pamoja na bonasi hizi kubwa, leo Tigo pia inatoa zawadi za shilingi milioni mbili na shilingi milioni moja kwa mawakala nane kutoka sehemu mbali mbali za nchi,’ aliongeza.
Hussein alibainisha kuwa jumla ya mawakala zaidi ya 73,000 wa Tigo Pesa walishiriki katika promosheni hiyo kote nchini. ‘Tunajivunia mchango wetu mkubwa katika kurahisisha upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha kwa watu wote nchini. Kupitia mtandao wetu mpana na uhakika wa mawakala wa Tigo pesa, tunaiwezesha jamii kutuma, kupokea na kufanya miamala ya fedha yenye mchango mkubwa katika uchumi wa watu binafsi, biashara, nchi na jamii yote kwa ujumla. Tigo Pesa ni zaidi ya huduma ya kutuma na kupokea pesa. Ni sehemu ya maisha.’
Tigo Pesa ni huduma ya fedha ya simu za mkononi ya pili kwa ukubwa nchini.
Kampuni ya Tigo ilianza kutoa huduma nchini Tanzania mwaka 1995 na kwa miaka mitatu mfululizo ndiyo kampuni ya simu inayokua kwa kasi zaidi nchini. Kwa sasa Tigo ndio kampuni ya simu za mkononi ya pili kwa ukubwa nchini inayohudumia wateja zaidi ya 11.6 milioni.
Tigo ni kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali nchini na inatoa huduma bora za kipekee za sauti, SMS na intaneti ya kasi ya juu ya 4G inayopatikana katika miji 24 nchini kote. Tigo pia inafahamika kwa promosheni kabambe na ofa bunifu kwa wateja wake.
0 comments:
Post a Comment