Hussein Makame-MAELEZO
USTAWI wa nchi yoyote duniani unategemea uwezo wa
kulinda mipaka yake na rasilimali muhimu zilizopo ili kunufaika nazo na kuweza
kupambana na maadui wake.
Katika kuhakikisha inatekeleza jukumu hilo kwa
uhakika, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), hivi karibuni lilizindua meli vita 2.
Meli hizo zilizopewa majina ya P77 PNS Mwitongo na P78
PNS Msoga, zimepatikana kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la JWTZ, Brigedia Generali
Rogastian Laswai anasema kupatikana kwa meli hizo ni tamati ya wazo lililodumu kwa
muda mrefu la wakuu waliopita wa kamandi hiyo waliobuni kutengeneza meli vita hizo.
Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange anasema meli hizo zimepatikana
kupitia utekelezaji wa dhana ya Tanzania kuwa na jeshi
dogo la kisasa linalotekeleza majukumu yake kwa ushupavu na weledi wa hali ya
juu.
“Utekelezaji wa dhana hii ni pamoja na ununuzi wa
zana na silaha mbalimbali za kivita, kuendeleza mafunzo ya kijeshi kulingana na
wakati, na kuboresha huduma muhimu kama vile makazi ya wanajeshi” anasema Jenerali Mwamunyange.
Anasema kuwa meli hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa
kulifanya jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Jakaya Kikwete anaamini itahakikisha
inaendelea kutekeza dhana hiyo.
Akizungumzia mchango wa China kwa jeshi hilo, Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi anasema Jeshi la Wanamaji
limeanzishwa rasmi mnamo mwaka 1971 kutokana na msaada wa Serikali ya Jamhuri
ya Watu wa China.
“Kwa kuanzia Serikali ya China ilitoa meli 13 na pia
walitujengea vituo vya rada kwa ajili ya uchunguzi wa pwani.Kuanzia mwaka 1971
China imekuwa ni msaada mkubwa ikiwemo ujenzi wa karakana na terezo ya
kuhudumia meli vita”anasema Waziri Dkt. Mwinyi.
Anasema hadi
leo Serikali ya Watu wa China imeendelea kuisaidia Tanzania kwa kuipatia meli
vita hizo, wataalamu kwa ajili ya karakana na kutoa nafasi nyingi za mafunzo
kwa maafisa na askari wa JWTZ.
Mbali na mchango huo, Waziri Dkt. Mwinyi anasema China
imeianzishia Combania ya Marine Special Forces pamoja na vifaa vya mafunzo na kuendelea
kuipatia walimu na wakufunzi kwa ajili ya shule ya Ubaharia iliyopo makao makuu
ya Kamandi ya Navy.
Anabainisha kuwa hizo zimekuja muda muwafaka
kutokana na mpango wa utafiti wa gesi na mafuta pamoja na kupambana na uharamia
baharini ambao siku za karibuni umekuwa ni tishio kwa taifa.
Anaongeza kuwa kupatikana kwa meli hizo kumezidisha
ari ya utendaji kazi kwa maafisa na askari wa kamandi ya Navy kwani sasa
wamepata uwezo wa kulinda mipaka ya Tanzania ya bahari kwa ufanisi zaidi.
“Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa
niaba ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na hususan Kamandi ya Navy, tunakushukuru
na kukupongeza Amiri Jeshi Mkuu kwa kuimarisha jeshi letu kwani uzinduzi wa leo ni kielelezo kingine tena cha dhamira na
jitihada madhubuti za kuliimarisha na kuliendeleza jeshi letu” anasema.
Anaongeza kuwa hadi sasa jeshi hilo limefanikiwa kupunguza
uharamia na uvuvi haramu, limewezesha maafisa na askari wa JWTZ kushiriki kwenye
operesheni mbalimbali na kuiletea sifa nzuri na heshima Tanzania.
Akizungumza kabla ya kuzindua meli hizo, Rais Jakaya
Kikwete ameishakuru Jamhuri ya Watu
wa China kwa kuiwezesha Tanzania kupata meli hizo.
“Ni ukweli usiofichika kuwa katika kuendeleza jeshi
letu hili hatuna mshirika anayefanana na Jamhuri ya Watu wa China.Wametusaidia
kwa mengi na ushirikino wetu sasa umekuwepo tangu Jeshi hili limeanza miaka 51
iliyopita mpaka leo hawajachoka” anasema Rais Kikwete.
“Kwa kweli hatuna maneno mazuri ya kuwashukuru zaidi
ya kusema ahsanteni sana.Tunatoa shukrani maalum kwa kampuni ya
Polytechonologies kwa ushirikiano wao.Hii ni moja ya kampuni ya China tunayoshirikiana
nayo katika kupata silaha za jeshi letu”.
Anasema kupatikana kwa meli hizo kunaandika historia
mpya katika Jeshi la Wanamaji kwani Kamandi ya Navy ya JWTZ imekuwa ikipata
msaada mbalimbali kutoka Jeshi la Ukombozi la China hadi sasa ingawa zipo nchi
nyingine zinazoisaidia Tanzania.
“Waswahili wanasema usione vyaelea vimeundwa, haya
yote ni matunda ya udugu na urafiki baina ya nchi zetu ulioanzishwa na
viongozi waasisi wa mataifa haya Rais Mao Zedong kwa upande wa China
na mwalimu Julias Nyerere kwa upande wa Tanzania.”
“Lakini pia viongozi waliowafuatia viongozi hao wa
China na Tanzanaia nao pia wameendelea kudumisha na kuendeleza uhusiano huo,
hayo ndio yametufikisha hapa tulipo.”
Rais Kikwete ameahidi kwamba ataendelea kuuenzi na kuudumisha
uhusiano huo wenye tija kubwa kwa nchi zote mbili.
Balozi wa China nchini Tanzania, LU Youqing anasema historia ya maendeleo ya nchi nyingine
duniani inaonesha kwamba ili kukabiliana na
matatizo ya ulinzi na usalama wa ndani na nje ya nchi ni lazima uwe na
jeshi lenye uwezo mkubwa wa kiulinzi.
Anasema ushirikiano wa majeshi kati ya Tanzania na
China ni sehemu muhimu sana kwa nchi husika kwani umekuwa nguzo kubwa ya
maendeleo ya nchi hizo.
“Kwa kweli
tunajisikia furaha sana kwa hilo na tunatoa pongezi zetu za dhati kwani hii
inaonesha kwamba urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania umepata
maendeleo makubwa sana” anasema Balozi Youqing.
“Nikiwa Balozi wa China nchini Tanzania mimi binafsi
nimeshuhudia ushirikiano mkubwa wa urafiki
mkubwa na udugu wa dhati na China na hii inaashiria kwa Wizara za Ulinzi ya
Taifa la China na Tanzania zimefanikiwa kuanzisha uhusiano mzuri” anaongeza.
Anasema wanaamini ushirikiano wa Jeshi la China na
Tanzania utaendelea kukua, Wizara ya Ulinzi ya China na Jeshi la China
litaendeleo kuunga mkono ujenzi na maendeleo ya Wizara ya Ulinzi ya Tanzania na
Jeshi la Tanzania”
“Meli vita hizi mbili zinaweza kutoa mchango wa
usalama na maendeleo ya Tanzania na hatimaye jeshi la wanamaji liwe na nguvu
zaidi.Udumu milele ushirikiano na urafiki kati ya China na Tanzania.”
Rais Kikwete anabainisha kuwa meli hizo ndio meli
kubwa kuliko zote ambazo Jeshi la Wanamaji linazo na kwamba zina uwezo wa
kwenda kwa kasi kubwa zaidi na kubeba silaha zenye nguvu zaidi.
“Moja ya kilio chetu cha muda mrefu ni uwezo mdogo
wa meli zetu na lengo letu ilikuwa ni kulipa uwezo jeshi letu kwa kupata meli
kubwa zenye uwezo wa kulinda mipaka yetu na rasilimali zetu kwenye maji
makubwa” anasema Rais Kikwete.
Baada ya kupata meli hizo Rais Kikwete anasema “Kwa
hiyo sasa tuna uwezo wa kulinda mipaka yetu ya bahari na mpaka wetu ni mrefu
una kilomita 1000 kutoka kule Moa mpaka unafika Msimbati ni maili 850 ambazo ni
sawa na kilomita 1000”
Anaongeza kuwa “Kwa hiyo huwezi ukaulinda kwa viboti
vidogo vidogo lazima uwe na meli kubwa kama hizi mbili na kuweza kujenga uwezo
wa kutosha.Kwa hiyo ndugu zetu wa China tunachoahidi ni kwamba tutaendelea
kushirikiana nanyi”
Anabainisha kuwa kabla ya kupata meli hizo Tanzania
imekuwa ikishirikiana na Kenya, Msumbiji na hata Afrika Kusini ili kulinda
mipaka na rasilimali zake.
Hivyo anasema sasa ana uhakika mpaka wa bahari wa
Tanzania utakuwa unalindwa kwa uhakika na rasilimali zake zitakuwa zinalindwa
kwa uhakika.
Naye Waziri Dkt. Mwinyi anasema meli hizo pia zitaongezea
uwezo wa JWTZ kutekeleza majukumu yake mbalimbali katika eneo la bahari ikiwa
ni pamoja na kupambana na maharamia.
“Pia meli
hizi zitasaidia kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia wakati wa majanga, kusaidia
kudhibiti uvuvi haramu pamoja na kutekeleza shughuli nyingine mbalimbali kwa
mahitajio ya kitaifa na kimataifa”, anasema Dkt. Mwinyi na kuongeza kuwa:
Hata hivyo, pamoja na kupata meli hizo Rais Dkt.
Kitwete anasema kuna mpango mwingine wa kupata meli vita nyingine kubwa zaidi
ya hizo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tuna kazi ya kutafuta meli
zenye uwezo huo lakini nataka kuwaambia kwamba tuna mpango tayari wa kupata
meli nyingine na baada ya muda si mrefu tunachozughulikia tu ni upatikanaji wa
fedha.Tukishakamilisha taratibu za kupata fedha kuna meli nyingine zitakuja
bora zaidi, kubwa zaidi na zenye uwezo mkubwa zaidi”
“Ni ghali
lakini lazima tuzichukue.Kwani kulinda uhuru ni kazi rahisi?Maana ukisema ni
gharama kupata vifaa hivyo hasara yake ndio hii, tunaibiwa samaki wetu, tuna
gesi asili, kule ipo siku watu wanaweza kwenda wakabomoa platform zile
wakatuibia rasilimali, hivyo lazima tujenge uwezo wa kuhakikisha kwamba tuna
uwezo wa kulinda mipaka yetu”.
Kama hiyo haitoshi anasema kuwa huo ni mwanzo wa
kufanya mambo makubwa kwa ajili ya Jeshi la Wanamaji kwani mipango imekamilika
ya kupata vyanzo vya fedha na anaamini kabla hajaondoka madarakani anaweza
kukukamilisha hilo.
Hivyo analitaka JWTZ na kuwamuru maafisa na askari
katika meli vita hizo kutekeleza majukumu yao kwa uhakika na uhodari wa hali ya
juu kwa kuzingatia na kufuata amri na maelekezo yaliyopo.
Pia wafuate maelekezo yatakayotolewa na viongozi wao
kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Ulinzi wa
Taifa na kanuni za majeshi ya Ulinzi.
Kwa mujibu wa JWTZ, meli hizo mbili zina mizinga
kisasa mikubwa miwili na mizinga ya msaada sita kwa kila meli na baadhi ya
mizinga hiyo inapiga kwa kutumia nguvu
ya umeme na vifaa maalum vya kutafutia shabaha vinavyoitwa GF 90.
Silaha za meli hizo husaidia katika mashambulizi ya
boti ndogo za maharamia ambazo zinaweza kuwa zinakaribia meli hiyo au kwa
chombo kingine tunachokwenda kutoa msaada baharini.
Mizinga hiyo yenye uwezo mkubwa ina uwezo wa kupiga shabaha
ya baharini kwa umbali wa kilometa 9, shabaha ya angani umbali wa kilometa 7.
Hivyo hiyo meli hii ina uwezo wa kufanya mapigano ya
angani, baharini na hata nchi kavu na zinaweza kusafiri kutoka bandari ya Dar
es Salaam hadi kwenye Economic Exclusive Zone ya Tanzania na ikaongeza umbali wa
mita 150 nautical miles.
Aidha zinaweza kwenda na kurudi eneo hilo kwa muda
wa siku saba baharini bila kuongeza mafuta, maji wala oil na kuwa na chakula
cha kutosha.
0 comments:
Post a Comment