Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
VIONGOZI wa vijiji, kata na wilaya, wametakiwa kuitisha vikao vya
kisheria kwa wakati, ili kutoa taarifa ya hali ya mambo yanavyoendelea
na hivyo kujenga imani na wananchi wanaowaongoza.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya
Nanyumbu, Salumu Palangyo, alipokuwa akitoa mada juu utawala bora
katika mdahalo wa mchakato wa katiba.
Alisema ni wajibu wa viongozi kutoa mrejesho kwa wananchi
wanaowaongoza na kwamba kushindwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na
utawala bora.
Mdahalo huo ulioandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali
Mkoa wa Mtwara (MRENGO) na kufadhiliwa na The Foundation for Civil
Society, ulijumuisha makundi mbalimbali yakiwemo ya walemavu, wastaafu,
wajane, vijana waliopo shuleni, vijiweni, madiwani na viongozi wa
kuchaguliwa na kuteuliwa.
Kaimu Katibu Tawala huyo aliwakumbusha viongozi kutoa mrejesho kwa
wanaowawakilisha kwa kufanya mikutano au kutoa taarifa katika mbao za
matangazo kwenye maeneo ya wazi.
“Ni wajibu wa viongozi kutoa mrejesho kwa wanaowaongoza… wewe kama ni
diwani au mbunge usipokuwa na utaratibu wa kutoa mrejesho maana yake
hutakuwa mwakilishi wa watu.
“Kwa upande wa vijiji mnatakiwa kufanya mikutano kila baada ya miezi
mitatu na kabla hujaenda kwenye vikao unatakiwa kupata maoni ya watu
wako na unaporejea pia wape kile kilichotokea kule,” alisema Palangyo.
Palangyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alieleza wananchi nao wana
wajibu wa kuhudhuria vikao na mikutano inayowahusu na kuwaeleza kuwa
wanapokuwa katika mikutano hiyo wana haki ya kuhoji na kupatiwa
ufafanuzi juu ya masuala ya fedha na miradi inayoendeshwa katika maeneo
yao.
Chanzo:Tanznia Daima
0 comments:
Post a Comment