Home » » Mzimu wa Mtwara waibuka tena

Mzimu wa Mtwara waibuka tena

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,Zelothe Stephen.
 
Huduma za kijamii katika Manispaa ya Mtwara na Mikindani mkoani Mtwara, jana zilisimama kutokana na wafanyabiashara kugoma kutoa huduma hizo wakidai kuwa walikuwa wanawakumbuka wananchi waliouawa na kujeruhiwa Mei 22, mwaka jana.
Tukio hilo lilitokana na vurugu za kupinga gesi asilia kusafirishwa kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyabiashara jana hawakufungua maduka yao na baadhi ya wamiliki magari kutotoa huduma za usafiri kwa madai ya kufanya dua maalum ya kumbukumbu za ndugu zao.

Hali hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wa manispaa hiyo na maeneo mengine kutoka na kukosa huduma ya usafiri na mahitaji muhimu yakiwamo vyakula.

NIPASHE lilitembelea maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara na kujionea sehemu kubwa ya mji huo huduma hizo zikiwa zimefungwa huku baadhi ya maeneo machache yakiendelea kutoa huduma.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na shule za msingi na NIPASHE ilifika katika baadhi ya shule na kujionea wanafunzi wakiwa wachache kutokana na wengi kushindwa kukosa usafiri na wengine kuhofia kuwapo kwa vurugu.

Kulwa Gambalama, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Raha Leo, alisema mahudhurio ya wanafunzi yaliathirika.

“Wanafunzi wachache wanaotoka maeneo ya Mbae na Chipuputa hawajafika shuleni…maduka ya vifaa vya shule yamefugwa na hivyo kufanya uongozi wa shule kushindwa kuchapisha mitihani,” alisema. 

Aidha, kutokana na hali hiyo, baadhi ya wazazi waliwazuia watoto wao kwenda shule kutokana na hofu ya kutokea vurugu kama mwaka jana.

“Asubuhi magari mawili ya polisi yalipita maeneo ya Coco Beach yakiwa na askari, nyuma ya magari hayo vilifungwa vitambaa vyekundu kuashiria hali ya hatari, hali hii ilinitia hofu  niliamua kumwambia mwanangu asiende shule,” alisema Chilumba Said, Mkazi wa Coco Beach.

USAFIRI

Wakazi wa maeneo ya Mbae, Chipuputa, Naliendele, Mpapura, Chuno, Kambarage, Magomeni, Mkangala na Mikindani walilazimika kukodi usafiri wa pikipiki kutokana na daladala zinakwenda katika maeneo hayo kusitisha huduma hiyo.

Filbert  Emmanuely, mkazi wa  Chipuputa alisema: “Hali ni mbaya hasa kwetu sisi wananchi tunaotegemea usafiri wa daladala, watoto wangu wanasoma Shule ya Msingi Lilungu, wamelazimika kutembea kwa miguu kwenda shule ili wakafanye mitihani yao ya majaribio,” alisema.

Aidha,  usafiri  kwenda wilaya za Newala, Tandahimba, Masasi na Lindi ulisitishwa na kuwalazimu wasafiri wa mkoa wa Lindi kupanda mabasi yanayokwenda Dar esSalaam.

“Kama ni kumbukumbu wangeendelea huku mambo mengine yakiendelea kama kawaida ikiwamo shughuli za uzalishaji,” alisema.

DC AELEZA CHANZO
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilmani Kapenjama, alisema mgomo huo ulisababishwa na baadhi ya watu waliokuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu tangu juzi jioni wakitisha watu wasifanye shughuli zozote za kijamii kwani ni siku ya kumbukumbu.

Alisema watu wote waliosambaza ujumbe huo baadhi yao wamekamatwa na wataendelea kuwakamata na kwamba watafikishwa katika vyombo vya sheria. Alisema  kitendo cha kufunga huduma za kijamii ni kinyume cha sheria.

Alisema watu hao wangeendelea kukumbuka ndugu zao, lakini si kushinikiza wafanyabiashara kufunga shughuli za kijamii na kuwagiza kufungua maduka na huduma zingine mara moja vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Pia aliwataka wananchi wa Mtwara wasiendelee kuwasikiliza watu wachache wenye kusambaza ujumbe huo usio na maana.

KAMANDA AKWEPA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alipoulizwa, hakutaka kulizungumzia tukio hilo zaidi ya kusema hali ya usalama ni shwari katika mkoa wake na kwamba kufungwa kwa huduma za kijamii hakumhusu na kushauri kuna wazungumzaji wengine wanaweza kulizungumzia.

Juzi askari polisi waliovalia sare na waliokuwa katika nguo za kiraia walionekana wakizunguka katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Ujumbe mfupi ambao NIPASHE iliona ulisomeka: “ Hii ni kwa wananchi wa Kusini wote  tarehe 22  mwezi Mei mwaka jana tulipoteza ndugu zetu kwa ajili ya sakata la gesi na kila palipo mwananchi wa Kusini Mmakonde na asiye Mmakonde, tutakuwa na maombolezo ya wahanga, hivyo maduka yatafungwa, daladala, usafiri wa pikipiki na bajaji, ukipata ujumbe huu isambaze kwa wengine, na hatutaogopa kuusambaza ujumbe huu.”

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wafanyabiashara  Soko Kuu (Wabisoco), Nyambi Nembo, alisema uamuzi wa wafanyabiashara hao ulifikiwa siku mbili kabla ya kusitisha huduma hiyo kwa kupeana taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu.

Nembo alisema hasara ya itakayopatikana ni kubwa na kwamba kwa jana walipoteza ushuru wa Sh. 150,000.

Katika sehemu zingine kama benki huduma ziliendelea, lakini wateja walikuwa wachache.

“Kweli huduma zipo na tunandelea na kazi, lakini hali ni tofauti kidogo ikilinganishwa na siku zingine, wateja hawaji na kwa sababu ya usafiri kwa kuwa wahusika wapo katika maombolezo,” alisema Meneja wa Benki ya Posta, Omary Kilimo.

Mei 22, 2013, vurugu kubwa zilitikisa Manispaa ya Mtwara Mikindani kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam hadi wananchi wa Kusini watakapohakikishiwa manufaa ya moja kwa moja ya gesi hiyo na kwamba haikustahili kuanza kunufaisha eneo jingine kabla ya maeneo yao.

Kutoka na vurugu hizo, watu watatu walifariki kwa kupigwa risasi, 18 kujeruhiwa kwa risasi, huku mali zikiharibiwa.

Baadhi ya mali hizo ni pamoja na Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kasim Mikongoro, nyumba za askari polisi, nyumba za mawaziri, viongozi wa CCM na wabunge.

Vurugu hizo zilitulia baada ya wanajeshi kupiga kambi kwenye mitaa mbalimbali ya mji huo na kufanya doria.

Pamoja na wanajeshi kuingilia kati, yalizuka mapambano  baina ya wananchi na polisi waliotuhumiwa kuchoma moto nyumba za raia na wananchi kuamua kulipiza kisasi.

Hali hiyo ilisababisha  baadhi ya viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema kukamatwa na baadaye Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji, kwa kudaiwa kuchochea virugu hizo.

Tangu wakati huo, serikali ilipiga marufuku shughuli zote za kisiasa hadi hali itakapotulia.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa