Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WIZARA ya Nishati na Madini imetoa sh milioni 48.42 kwa ajili ya
kuwalipia ada wanafunzi 40 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, wanasoma
kwenye Chuo Kikuu cha Stella Maris.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Mtwara,
Mkuu wa Kitengo cha Falsafa na Maadili ya Chuo Kikuu cha Stella Maris
Mtwara, Mchungaji Dk. Aidan Msafiri alisema kilichofanywa na wizara
hiyo ni majibu ya ombi la kuwahamasisha wakazi wa mikoa hiyo wasiende
mbali kutafuta elimu ya chuo.
Alisema alipokuwa akiwasilisha kwenye kongamano la viongozi wa dini
mbalimbali lililofanyika mjini hapa hivi karibuni ambapo Katibu Mkuu wa
wizara hiyo Eliakim Maswi alishiriki, aliiomba wizara kuwasomesha
wanafunzi 20 kutoka Lindi na wengine Mtwara.
“Wakati nawasilisha mada yangu katika kongamano lile, nilitoa
changamoto na kuiomba wizara iwasomeshe wanafunzi 20 kutoka Lindi na
Mtwara ili kuwahamasisha wengine wasiende nje ya mkoa huu kutafuta
vyuo. Hapa walimu wazuri.
“Baada ya ombi hilo katibu mkuu wa wizara alijibu hoja yangu kwa
kukubali ombi langu na tayari wanafunzi hao wameanza masomo, kati yao
wanafunzi 36 wanasoma ngazi ya cheti na wanne wanasoma diploma,”
alisema.
Alisema baada ya hilo walitangaza na kwa bahati nzuri mwamko wa
wanafunzi na wananchi wa Mtwara na Lindi ulikuwa mara mbili yake kwani
aliomba wasomeshwe wanafunzi 20, lakini maombi yalipelekwa 40.
“Ilikuwa changamoto kwa wizara baada ya kupeleka majina 40 badala ya
20 niliyoomba mwanzo, lakini halikuwa jambo baya ila nashukuru wizara
hii ilikubali kuwasomesha wanafunzi wote 40. Naomba wizara nyingine
ziige mfano huu,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment