Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
NAHODHA wa timu iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Ndanda
FC ya mkoani hapa, Salum Hamisi ‘Gallas’, amewataka wachezaji wenzake
wasiwe na tabia ya papara kutaka kucheza timu kubwa kama Yanga na Simba,
kwani zimekuwa zikiua vipaji vya wachezaji wadogo.
Wito huo ameutoa jana wakati akizungumza na Tanzania Daima
kwa njia ya simu na kubainisha kwamba hawapaswi kubabaika na timu kubwa,
kwa sababu leo wakitoka Ndanda kwenda Yanga ama Simba, watasajiliwa
vizuri, lakini itakuwa ngumu kupata nafasi ya kucheza na kuonekana
zaidi.
“Tusiwe na papara na wala tusidanganyike kwa sababu tu ni klabu
kubwa, lakini zinatumaliza sisi wachezaji wadogo, kwa sababu leo ukitoka
hapa kwenye timu yako ya Ndanda kwenda Yanga au Simba, umesajiliwa
vizuri, lakini huwezi kupata nafasi ya kucheza ili uonekane zaidi, sana
sana watakuwa wanakiua kipaji chako cha uchezaji, kwani unapokaa bila
kucheza kwa muda mrefu na kipaji kinapotea,” alisema Gallas.
Pamoja na mambo mengine, Gallas alisema kuwa kitu ambacho wamekifanya
hadi kupata mafaniko ya kupanda daraja ni kujituma na uvumilivu ndani
ya timu yao.
“Kitu kikubwa ambacho kimetufanya hadi kupata mafanikio ya kupanda
daraja, ni kujituma na uvumilivu ndani ya timu na kuwasikiliza viongozi
wetu walivyokuwa wanatuambia, hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio yetu,”
alisema.
Nahodha huyo aliwaomba wapenzi na mashabiki wa Ndanda FC, wasiache
hamasa ambayo wameifanya kwa kuwashangilia na kuwafuata kila walipokuwa
wanacheza, bali waendelee nayo kwani imewahamasisha na kufanya vizuri.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment