Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Bw.Mrimia
Mchomvu (kushoto) akiongea na Viongozi wa Dini kutoka mikoa ya
Lindi na Mtwara waliofika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini,
kabla ya kuanza ziara ya mafunzo ya gesi asilia na Mafuta nchini
Thailand.Kushoto kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu ni
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati
na Madini, Bw. Maseke Mabiki.
Baadhi ya Viongozi wa Dini watakaohudhuria mafunzo kuhusu Gesi asilia
na Mafuta wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika
Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Mrimia Mchomvu (hayupo pichani).
Na Teresia Mhagama
Jumla ya Viongozi 19 wa Dini kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajia kwenda nchini Thailand kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka huu kwa ajili ya ziara ya mafunzo katika masuala ya gesi asilia na mafuta.
Jumla ya Viongozi 19 wa Dini kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajia kwenda nchini Thailand kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka huu kwa ajili ya ziara ya mafunzo katika masuala ya gesi asilia na mafuta.
Ziara hiyo inatokana na juhudi za serikali katika kuhakisha elimu
kuhusu masuala ya gesi asilia na mafuta inatolewa kwa wananchi
wa kada mbalimbali ili waweze kufahamu mchakato mzima wa
upatikanaji wa gesi asilia na mafuta, faida zake katika nyanja za
kiuchumi na kijamii, changamoto zake na namna nchi nyingine
zinavyotumia rasilimali hiyo katika kukuza uchumi.
Akiwaaga viongozi hao kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
Watu katika Wizara hiyo, Bw. Mrimia Mchomvu amesema kuwa
Wizara ya Nishati na Madini imeratibu mafunzo hayo ili kujenga
uelewa kwa viongozi hao ambao nao wataitumia elimu hiyo katika
kuwaelimisha wananchi kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini
ili kujenga uelewa wa pamoja utakaowafanya wananchi kushiriki
na kuwa na mtazamo chanya kuhusu miradi mbalimbali ya gesi
asilia nchini.
Bw. Mrimia Mchomvu ameeleza kuwa Serikali imeamua
kuwapeleka viongozi hao nchini Thailand kwa kuwa nchi hiyo
imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kujipanga vizuri
katika kutumia gesi asilia katika masuala mbalimbali ya kiuchumi
na kuhakikisha wananchi wanafaidika na uwepo wa gesi hiyo.
Naye mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la
Waislam Tanzania (BAKWATA), Sheikh Said Sinani akiongea
kwa niaba ya viongozi hao wa dini wanaokwenda nchini Thailand,
aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kushirikisha viongozi
wa dini katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
Amesema kuwa viongozi hao wa dini watahudhuria mafunzo
hayo kwa umakini mkubwa na baada ya kupata uelewa mpana
kuhusu gesi asilia na mafuta kutoka nchi nyingine, watakuwa
mabalozi katika kutoa elimu kwa waumini wao ili kujenga uelewa
wa pamoja kuhusu sekta hiyo nchini.
Pamoja na kujifunza masuala ya gesi asilia na mafuta nchini
Thailand, viongozi hao watapata fursa ya kutembelea eneo
maalum la viwanda ambalo ukuaji wake umetokana na kuwepo
kwa gesi asilia, Shirika la Umma linalojishughulisha na masuala
ya Gesi na Mafuta, Mamlaka ya Uzalishaji Umeme, Mamlaka ya
Usambazaji Umeme, mtambo wa kuzalisha umeme unaotokana
na Tungamotaka (Biomass), mtambo wa umeme wa jua, na
mtambo wa umeme wa Bayogesi.
Viongozi hao wa Dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajia kurejea
nchini mnamo tarehe 07 Mei, 2014.
0 comments:
Post a Comment