Home » » MADEREVA BODABODA WAGOMA

MADEREVA BODABODA WAGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
MADEREVA pikipiki ‘bodaboda’ mkoani Mtwara jana waligoma kubeba abiria kupinga kitendo cha askari polisi wa kikosi cha kuzuia fujo (FFU) kuwakamata na kuwapiga bila sababu za msingi.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano dereva wa bodaboda, Rashidi Mwarabu mkazi wa India Kotazi, alisema sababu za mgomo huo jana ni kupinga unyanyasaji wa polisi.
“Kitendo tunachofanyiwa na polisi hatukikubali… wanatuona sio binadamu wenzao, wanafukuza barabarani na wakikukamata wanakupiga na kukunyang’anya pikipiki, wakikupeleka kituoni wanakubambikia makosa.
“Wangetuambia kama kuna tatizo, lakini sio kila unapokutana nao barabarani hawakuulizi kitu wanaanza kutufukuza na wakati mwingine wamekuwa wakisababisha ajali, wakikuta pikipiki zimepaki sehemu wanazichukua na kuzipakia kwenye gari na kuondoka nazo kituoni,” alisema.
Juma Hamisi, mkazi wa Magomeni, alisema kitu kikubwa kinachowaumiza ni askari hao kuonyesha uonevu uliopitiliza, huku akibinisha kwamba wangekuwa wanawasimamisha na kuwahoji ili wajue makosa yao, lakini askari hao hawafanyi hivyo jambo linalosababisha uadui kati ya polisi na raia.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Zelothe Stephen, alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi kuzungumzia suala hilo alisema ametingwa na kazi hadi atakapomaliza kisha kukata simu.
  Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa